Qatar yawalaumu viongozi wa nchi za Kiarabu kwa siasa za kinafiki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amelaani mashambulizi yanayofanywa dhidi ya maeneo ya raia katika mji mkuu wa Libya Tripoli na kusisitiza kuwa, unafiki wa kisiasa na undumilakuwili ni mambo ambayo yameuchosha ulimwengu wa Kiarabu na ndiyo yanayochochea vitendo vya kigaidi.
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Aal Thani alisema hayo jana (Jumatatu) katika ukurasa wake wa Twitter na huku akiyaita ni mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na Jenerali Khalifa Haftar katika maeneo ya makazi ya raia huko Tripoli, mji mkuu wa Libya amesema kuwa, lengo la kuwashambulia raia na watu wa kawaida ni kuzusha vurugu na kwamba kushambulia taasisi muhimu za huduma za jamii ni jinai ya kivita ambavyo inabidi watendaji wake na waungaji mkono wao wabebe dhima na lawama zote.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ameongeza kuwa, baadhi ya nchi zinadai tu kupambana na ugaidi lakini kwa hakika zinatumia ugaidi kufanya vitendo vya kigaidi dhidi ya wananchi na mataifa ya Kiarabu.
Jenerali Khalifa Haftar ambaye ni mkuu wa wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya alianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya Tripoli tarehe 4 mwezi huu wa Aprili baada ya kufanya safari ya siku moja mjini Riyadh na kuonana na viongozi wa Saudi Arabia. Mashambulizi ya jenerali huyo muasi yalianza baada ya kuzungumza kwa simu na rais wa Marekani, Donald Trump.