Viongozi wa Iraq wamwambia Pompeo, Baghdad itaendelea kuwa rafiki wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53352-viongozi_wa_iraq_wamwambia_pompeo_baghdad_itaendelea_kuwa_rafiki_wa_iran
Waziri Mkuu na Rais wa Iraq wamemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwamba Baghdad itaendelea kuimarisha ushirikiano, urafiki na majirani wake ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 08, 2019 12:23 UTC
  • Viongozi wa Iraq wamwambia Pompeo, Baghdad itaendelea kuwa rafiki wa Iran

Waziri Mkuu na Rais wa Iraq wamemwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kwamba Baghdad itaendelea kuimarisha ushirikiano, urafiki na majirani wake ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Jumanne usiku, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika safari ya ghafla na ya masaa machache aliwasili mjini Baghdad na kukutana na Adil Abdul-Mahdi, Waziri Mkuu na Barham Salih, Rais wa Iraq ambapo alipata kuzungumza nao kwa nyakati tofauti. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq imesema katika mazungumzo ya pande mbili, Adil Abdul-Mahdi alimwambia Pompeo kwamba, uhusiano wa kigeni wa Iraq unapewa kipaumbele cha kwanza katika maslahi ya kitaifa.

Marekani na njama zake za kila upande dhidi ya Iran

Aidha ofisi ya rais wa Iraq nayo imetoa taarifa ikisema kuwa, katika mazungumzo na Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani, Barham Salih amemuhakikishia kwamba licha ya Baghdad kuwa na ushirikiano na Washington, lakini itaendelea kufungamana na urafiki wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Salih ameongeza kwamba, Iraq inautambua uhusiano wa kigeni kuwa uliosimama katika msingi wa maslahi ya kitaifa, kama ambavyo Baghdad itaendeleza juhudi zake za kupanua ushirikiano na nchi nyingine ikiwemo Iran. Duru za habari zimearifu kwamba safari ya ghafla na ya muda mfupi ya Mike Pompeo nchini Iraq, ilikuwa na lengo la kueneza chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.