Jordan yaombwa isishiriki mkutano wa Marekani nchini Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i53634-jordan_yaombwa_isishiriki_mkutano_wa_marekani_nchini_bahrain
Serikali ya Jordan imetakiwa kutoshiriki mkutano wa Marekani wenye lengo la kuzindua hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa 'Muamala wa Karne' unaotazamiwa kufanyika mwezi ujao wa Juni nchini Bahrain.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 21, 2019 23:13 UTC
  • Jordan yaombwa isishiriki mkutano wa Marekani nchini Bahrain

Serikali ya Jordan imetakiwa kutoshiriki mkutano wa Marekani wenye lengo la kuzindua hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa 'Muamala wa Karne' unaotazamiwa kufanyika mwezi ujao wa Juni nchini Bahrain.

Mwito huo ulitolewa jana Jumanne na tawi la kisiasa la harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Jordan ambalo limesisitiza kuwa, mkutano huo ni sehemu ya njama za kuyeyusha kadhia ya Palestina.

Taarifa ya harakati hiyo ya muqawama wa Kiislamu imesema kuwa, "Maafisa wa serikali ya Jordan katika ngazi zote hawapaswi kuunga mkono makubaliano yoyote ambayo yanakanyaga haki za Wapalestina na maslahi ya taifa la Jordan."

Mounir Rashid, mwanachama wa vuguvugu la Islamic Action Front ambalo ni tawi la kisiasa la Ikhwanul Muslimin ya Jordan amesema, mkutano huo ujao wa Marekani nchini Bahrain ni mkakati mpana wenye lengo la kuitokomeza kikamilifu kadhia ya Palestina, unaokwenda sambamba na sera batili za Rais Donald Trump wa Marekani.

Mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jared Kushner hivi karibuni alifichua kuwa, hatua ya kwanza ya 'Muamala wa Karne' itazinduliwa na Marekani nchini Bahrain katika 'Kongamano la Kiuchumi' litakalofanyika Juni 25 na 26.

Wakimbizi wa Kipalestina nchini Jordan

Mwezi uliopita, ujumbe wa kibiashara na kisiasa wa utawala wa Kizayuni wa Israel ulishiriki kwa siri kubwa Mkutano wa Kimataifa wa Kiuchumi wa Manama nchini Bahrain licha ya waandalizi wa mkutano huo kudai kuwa Wazayuni hao hawangeushiriki kutokana na sababu za kiusalama.

Wapalestina wamekuwa wakiulaani na kuupinga vikali mpango huo wa 'Muamala wa Karne' wakiutaja kuwa ni moja ya njama kubwa zaidi dhidi ya taifa madhulumu la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.