Answarullah: Operesheni za droni dhidi ya Saudia na Imarati zitaendelea
Mohamed Albakhiti, Mjumbe wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Wananchi ya Answarullah nchini Yemen, amesema kuwa operesheni za kikosi cha anga na ndege zisizo na rubani (droni) zitaendelea hadi pale Saudia na Imarati zitakapohitimisha uvamizi wao.
Sambamba na kubainisha kwamba operesheni za ndege zisizo na rubani zinatekelezwa katika fremu ya ulinzi wa Yemen, Albakhiti ameongeza kwamba Saudia haina chaguo jingine ghairi ya kurudi nyuma na kukomesha uvamizi wake dhidi ya Yemen. Aidha Albakhiti, ameyaonya mashirika ya anga ya kiraia ya nchi za wavamizi kwamba, viwanja vya ndege vya Saudia viko katika shabaha halali na ya kisheria ya mashambulizi ya jeshi la Yemen. Hayo yanajiri katika hali ambayo kamati za wananchi wa Yemen jana ziliushambulia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abha, kusini mwa Saudia kwa kutumia ndege tano zisizo na rubani na kusababisha uharibifu mkubwa.
Katika hatua nyingine Badr Kalshat, kaimu mkuu wa jimbo la Al Mahrah nchini Yemen amefichua hali ya mambo ndani ya jela za siri za muungano vamizi wa Saudia na Imarati katika mji wa Al Ghaydah na vitendo vya utesaji mkubwa dhidi ya mateka wasio na hatia kwenye jela hizo na kuitaka serikali iliyojiuzulu ya Yemen kutoa amri ya kufanyika uchunguzi kuhusiana na jinai hizo sambamba na kufungwa kwake mara moja. Saudia na Imarati zinaendelea kufanya jitihada za kupenya na kujitanua zaidi ndani ya jimbo la Al Mahrah, mashariki mwa Yemen kupitia kutuma vibaraka wao jimboni humo.