Answarullah: Kuna vita vikubwa vinakuja ndani ya ardhi ya Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54144-answarullah_kuna_vita_vikubwa_vinakuja_ndani_ya_ardhi_ya_saudi_arabia
Mjumbe mmoja mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Answarullah ya Yemen amesema kuwa, karibuni hivi kutaanza vita vikubwa ndani ya ardhi ya adui Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 16, 2019 02:18 UTC
  • Answarullah: Kuna vita vikubwa vinakuja ndani ya ardhi ya Saudi Arabia

Mjumbe mmoja mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Answarullah ya Yemen amesema kuwa, karibuni hivi kutaanza vita vikubwa ndani ya ardhi ya adui Saudi Arabia.

Televisheni ya al Alam imemnukuu Muhammad Nasir al Bukheiti, mmoja wa wajumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Answarullah ya Yemen akisema katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, ni haki ya wananchi wa Yemen kumshambulia adui ndani ya ardhi yake na kumsababishia hasara kama alizowasababishia wananchi hao.

Juzi Ijumaa pia al Bukheiti aliyaonya mashrika ya ndege na yasiyo ya kijeshi kuacha kutuma ndege zao katika viwanja vya ndege vya Saudi Arabia akitahadharisha kuwa viwanja hivyo hivi sasa ni shabaha ya mashambulizi ya jeshi la Yemen.

Hivi karibuni jeshi la Yemen liliupiga kwa kombora la Cruise, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abha wa kusini mwa Saudi Arabia

 

Kwa upande wake gazeti la al Quds al Arabi limeandika kuwa,: Onyo hilo la al Bukheiti linaonesha kuweko mabadiliko katika mlingano wa kivita kwa manufaa ya jeshi na Answarullah huko Yemen.

Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo limefanya mashambulizi mengi ndani ya ardhi za Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwa kutumia makombora na droni (ndege zisizo na rubani) na kuwasababishia hasara kubwa wavamizi hao wa Yemen.

Tangu mwezi Machi 2015 hadi hivi sasa Saudia inaongoza muungano vamizi wa nchi za Kiarabu hasa Imarati kufanya jinai kubwa dhidi ya wananchi wa Yemen na wamesababisha hasara kubwa kwa raia maskini wa Yemen na kuharibu kabisa miundombinu na maeneo ya huduma za jamii ya nchi hiyo ya Kiarabu.