Hizbullah: Utatuzi wa kadhia ya Palestina kwa fedha ni udhalilishaji mkubwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54338-hizbullah_utatuzi_wa_kadhia_ya_palestina_kwa_fedha_ni_udhalilishaji_mkubwa
Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Muqawama ya nchini Lebanon Hizbulla, amesema kuwa, mtazamo wa Marekani kwa wananchi wa Palestia kuwa ni watu masikini ambao matatizo yao yanatatuliwa tu kwa fedha, ni udhalilishaji mkubwa kwa watu wa taifa hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2019 23:06 UTC
  • Hizbullah: Utatuzi wa kadhia ya Palestina kwa fedha ni udhalilishaji mkubwa

Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Muqawama ya nchini Lebanon Hizbulla, amesema kuwa, mtazamo wa Marekani kwa wananchi wa Palestia kuwa ni watu masikini ambao matatizo yao yanatatuliwa tu kwa fedha, ni udhalilishaji mkubwa kwa watu wa taifa hilo.

Ibrahim Amin al-Sayyed amesema kuwa kadhia ya Palestina ni kadhia kubwa katika ulimwengu wa leo, lakini kitendo cha Marekani kuwapuuza Wapalestina, haki ya uepo wao na haki yao ya kisiasa, kimeifanya iwatazame Wapalestina kama ni kundi la watu masikini ambao matatizo yao yanaweza kutatuliwa kifedha kupitia kikao cha mjini Manama, Bahrain. Kwa upande wake 'Jopo Kazi la Lebanon na Palestina' linalofuatilia kadhia ya wakimbizi wa Kipalestina, jana Jumatatu lilifanya kongamano nchini Lebanon kwa lengo la kutangaza msimamo wake kuhusiana na kadhia ya Muamala wa Karne. Kikao cha mjini Manama chenye lengo la kuchunguza njia za utekelezaji wa hatua ya kwanza ya mpango wa Kimarekani na utawala wa Kizayuni wa Muamala wa Karne, kuhusiana na kadhia ya Palestina kimepangwa kuanza leo Jumanne  na kumalizika siku ya Jumatano.

Ibrahim Amin al-Sayyed, Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Muqawama ya Hizbulla nchini lebanon

Mpango wa Muamala wa Karne ambao ulibuniwa na Rais Donald Trump wa Marekani, huku Jared Kushner, mkwe wa rais huyo akiwa mtekelezaji wake mkuu unalenga kuikabidhi nusu nzima ya eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Quds kwa utawala haramu wa Kizayuni, na badala yake mji wa Abu Dis ndio utafanywa kuwa mji mkuu wa Palestina badala ya mji wa Quds. Aidha kwa mujibu wa mpango huo, wakimbizi wa Kipalestina wanaoishi katika nchi tofauti, hawatokuwa na haki ya kurejea katika ardhi zao asilia, kama ambavyo Wapalestina watakabidhiwa ardhi iliyosalia katika eneo la Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, suala ambalo limepingwa na kila pande ndani na nje ya Palestina