Hamas yaapa kudumaza mpango wa Trump wa "Muamala wa Karne"
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema kuwa itaendeleza harakati za kupinga mpango eti wa amani uliozusha makelele mengi wa Rais Donald Trump wa Marekani baina ya utawala haramu wa Israel na Wapalestina uliopewa jina la "Muamala wa Karne"
Khalil al-Hayya ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa harakati ya Hamas amesema kuwa, Wapalestina wanaweza kukabiliana na kuzima njama zote zinazokusia kuharibu kadhia yao ya kitaifa na kwamba Hamas itayakutanisha pamoja makundi yote ya Kipalestina kwa ajili ya kuzima njama zote zinazofanywa dhidi ya taifa la Palestina.
Hayya ameongeza kuwa, kongamano la kiuchumi lililodhaminiwa na Marekani nchini Bahrain mwishoni mwa mwezi uliopita kwa ajili ya kuzindua mpango wa Muamala wa Karne lilifeli kabla hata halijaanza kutokana na kususiwa na Wapalestina.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Hamas ametilia mkazo udharura wa kuwepo umoja na mshikamano baina ya makundi yote ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na njama kama ile ya kongamano la Bahrain na amepongeza misimamo ya baadhi ya nchi na mataifa ya Waislamu dhidi ya kongamano hilo.
Wakati huo huo mkuu wa Idara ya Siasa ya Hamas, Ismail Hania amemshukuru Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri kwa msimamo wake wa kukataa mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani uliopigiwa debe sana na vilevile kongamano la Bahrain.
Kongamano la Bahrain la kuzindua mpango wa Muamala wa Karne lilifanyika tarehe 25 na 26 mwezi uliopita wa Juni nchini Bahrain. Mkutano huo ulisusiwa na makundi yote ya Wapalestina, suala ambalo lilizusha maswali mengi juu ya uhalali wake na kuufanya upoteze maana na kugonga mwamba.