Walowezi wa Kizayuni wavamia tena Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa
Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameuvamia tena Msikiti wa al-Aqswa huko Palestina wakisaidiwa na askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu na kibla cha kwanza cha Waislamu.
Vyombo vya habari vya Palestina vimetangaza kuwa, walowezi hao baada ya kuingia katika msikiti huo walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, vitendo vya walowezi wa Kizayuni vya kuuvamia msikiti mtakatifu wa al-Aqswa na kuuvunjia heshima vimeongezeka mno katika miezi ya hivi karibuni.
Inaelezwa kuwa, katika mwezi uliopita wa Juni pekee, walowezi wa Kizayuni waliuvamia msikiti huo mara 2800 na kufanya vitendo vya kulivunjia heshima eneo hilo takatifuu.
Kwa mujibu wa duru za kipalestina, karibu kila siku walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakifanya uvamizi katika msikiti huo lengo likiwa ni kutekeleza njama za kutokomeza utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa Msikiti wa al-Aqswa na badala yake kuweka nembo za Kizayuni.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.
Hata hivyo kusimama kidete wananchi wa Palestina hadi sasa kumekwamisha njama na mipango yote ya Wazayuni, zikiwemo njama zake za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul Muqaddas.