Umoja wa Falme za Kiarabu wataka kuanza mazungumzo kuhusu Yemen
(last modified Sun, 11 Aug 2019 03:46:40 GMT )
Aug 11, 2019 03:46 UTC
  • Umoja wa Falme za Kiarabu  wataka kuanza mazungumzo kuhusu Yemen

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu ametaka kuanza mazungumzo kwa ajili ya kuhitimisha hali ya mvutano katika mji wa Aden na kurejesha amani kusini mwa Yemen.

Abdullah bin Zayed al Nahyan amewasilisha ombi hilo kwa Martin Griffith Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Yemen ili atafute njia ya kusimamishwa mapigano katika mji wa Aden huko Yemen. Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati amewasilisha ombi hilo kufuatia kuongezeka hitilafu  kati ya vibaraka wanaoungwa mkono na Imarati na Saudi Arabia huko Aden.

Mamluki wa Kisudan nchini Yemen

Muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudia kwa kushirikiana na Imarati siku hizi unaendesha vita vya niaba na kutekeleza mauaji kusini mwa Yemen baada ya kupita zaidi ya miaka minne ya vita na umwagaji damu katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Mapigano kati ya vikosi vitiifu kwa baraza la mpito huko kusini mwa Yemen vyenye mfungamano na Imarati; na vikosi vya Abdu Rabbuh Mansour Hadi Rais wa Yemen aliyejiuzulu vinavyoungwa mkono na Saudia yamepamba moto tangu Agosti Mosi mwaka huu. Aidha makumi ya mamluki hao wameuliwa na kujeruhiwa.