Iraq yavunja mtandao wa kigaidi kuelekea Arubaini ya Imam Hussein AS
Vyombo vya usalama nchini Iraq vimefanikiwa kuvunja mtandao wa kigaidi uliokuwa unakula njama ya kutekeleza mashambulizi ya kigaidi wakati wa Arubaini ya Imam Hussein (AS).
Ofisi ya Habari za Usalama ya Iraq imesema katika taarifa kuwa, maafisa usalama katika mji wa Samarra, kaskazini mwa mji mkuu Baghdad wametibua njama za genge moja la kigaidi lenye watenda jinai sita, waliokuwa wanapanga namna ya kufanya mashambulizi dhidi ya Mazuwwar wakati wa Arubaini ya Imam Hussein (AS).
Mmoja wa magaidi hao waliotiwa nguvuni na maafisa usalama wa Iraq ni mke wa gaidi sugu wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) aliyeko Syria. Arubaini ya mwaka huu inatazamiwa kuadhimishwa kati ya Oktoba 19 na 20.

Hapo awali, serikali ya Baghdad ilitangaza kuwa imewakamata watu 78 tokea Agosti mwaka huu, wakihusishwa na njama za kufanya hujuma za kigaidi wakati wa Ashura ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW katika mji mtukufu wa Karbala.
Mamilioni ya wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW humiminika nchini Iraq kila mwaka kutoka kona zote za dunia kwa ajili ya kuadhimisha Arubaini ya Imam Hussein AS.