Walowezi 200 wa Kizayuni wavamia Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa
Walowezi wapatao 200 leo wamevamia Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa wakiitikia wito wa makuhani wa utawala ghasibu wa Israel huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Uvamizi wa walowezi hao ambao umefanyika kwa msaada wa askari wa jeshi la utawala haramu wa Israel na kuuvunjia heshima msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu uliwashirikisha pia Wabunge kadhaa wa Bunge la utawala ghasibu wa Israel.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, vitendo vya walowezi wa Kizayuni vya kuuvamia msikiti mtakatifu wa al-Aqswa na kuuvunjia heshima vimeongezeka mno katika miezi ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa duru za Kipalestina, karibu kila siku walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakifanya uvamizi katika msikiti huo lengo likiwa ni kutekeleza njama za kutokomeza utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa Msikiti wa al-Aqswa na badala yake kuweka nembo za Kizayuni.

Katika miaka ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha hujuma na uvamizi wake dhidi ya maeneo ya Wapalestina ukifanya njama za kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.
Hata hivyo kusimama kidete wananchi wa Palestina hadi sasa kumekwamisha njama na mipango yote ya Wazayuni, zikiwemo njama zake za kubadilisha muundo wa kijamii na kijiografia wa Baytul Muqaddas.
Uvamizi huo unakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina.