Jihadul-Islami: Muqawama umesambaratisha njama za utawala wa Kizayuni
Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islam ya Palestina amesema kuwa, muqawama umesambaratisha njama za utawala vamizi wa Kizayuni.
Ziyad Al-Nakhaleh ameyasema hayo alipokutana na jamii ya maulama wa Kiislamu nchini Lebanon mjini Bairut ambapo sambamba na kupongeza nafasi ya Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu katika kuunga mkono muqawama na kupambana na wavamizi wa Kizayuni, ameongeza kuwa, hii leo muqawama una nguvu kuliko wakati mwingine wowote. Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islam ya Palestina amebainisha kwamba katika hali ambayo baadhi ya nchi za eneo la Asia Magharibi zinafanya jitihada za kujikurubisha kwa utawala haramu wa Israel, lakini wanamapambano wa Lebanon na Palestina wamesimama imara dhidi ya njama za utawala huo ghasibu wa Kizayuni.
Katika mkutano huo, Sheikh Hassan Bin Abdallah, Mkuu wa Kamati ya Kiidara ya Jumuiya ya Maulama wa Kiislamu nchini Lebanon ameipongeza harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina kutokana na kulinda itibari, uthabiti na nafasi yake na kusema kuwa, harakati hiyo kamwe haitofanya mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.