Waziri Mkuu wa Lebanon Saad al Hariri amejiuzulu
Waziri Mkuu wa Lebanon Saad al Hariri ametangaza kujiuzulu huku nchi hiyo ikiwa imegubikwa na maandamano ya wananchi.
Saad al Hariri ametoa tangazo hilo mjini Beirut leo alasiri wakati akihutubu kwa njia ya moja kwa moja kupitia televisheni hii ikiwa ni mara ya pili kulihutubia taifa tokea maandamano yaanze nchini humo.
Al Hariri amesema, "daima kumekuwa na jitihada za kuilinda nchi lakini leo mchakato huo umefika katika mkwamo." Hariri amemkabidhi Rais Michel Aoun barua yake ya kujiuzulu.
Saad al Hariri alichaguliwa kuwa waziri mkuu mnamo Disemba 2016 na Novemba mwaka 2017 akiwa safarini Saudi alitekwa nyara na wakuu wa nchi hiyo na kulazimihswa kutangaza kujiuzulu kwa njia ya televisheni ya utawala wa Saudia. Lakini punde baada ya kuondoka Saudia alitangaza kubatilisha uamuzi wake wa kujiuzulu.
Baada ya uchaguzi wa bunge Mei 2018, kwa mara nyingine Hariri aliteuliwa kuwa waziri mkuu na sasa baada ya miezi 17 amejiuzulu kufuatia maandamano ya wananchi.
Tokea Oktoba 17 hadi sasa, Lebanon imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya wananchi wanaolalamikia ongezeko la kodi na ushuru pamoja na mgogoro wa kiuchumi nchini humo.