Marekani yadai imeitupa baharini maiti ya Abu Bakr al Baghdadi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56932-marekani_yadai_imeitupa_baharini_maiti_ya_abu_bakr_al_baghdadi
Mkuu wa majeshi ya Marekani amedai kuwa mwili wa aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr al Baghdadi umetupwa bahaini baada ya kuthibitishwa kuwa wake kupitia kipimo cha vinasaba (DNA).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 29, 2019 16:36 UTC
  • Marekani yadai imeitupa baharini maiti ya Abu Bakr al Baghdadi

Mkuu wa majeshi ya Marekani amedai kuwa mwili wa aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr al Baghdadi umetupwa bahaini baada ya kuthibitishwa kuwa wake kupitia kipimo cha vinasaba (DNA).

Jenerali Mark A. Milley amedai katika mkutano wa waandishi habari kwamba jeshi la Marekani limechukua picha na filamu nyingi kuhusiana na operesheni ya kuua al Baghdadi, mwenendo wa kuthibitisha utambulisho wake na picha za mabaki ya mwili wake na kuongeza kuwa: Washington inazihifadhi picha na filamu hizo kwa sasa.

Matamshi haya ya kamanda wa majeshi ya Marekani yametolewa siku moja baada ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo kutangaza kwamba askari wa kikosi maalumu cha jeshi la nchi hiyo wamemuangamiza kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh katika oresheni iliyofanyika Idlib huko kaskazini magharibi mwa Syria. 

Itakumbukwa kuwa mwaka 2011 pia Marekani ilitangaza kuwa, imemuua kiongozi wa kundi la kigaidi la al Qaida, Usama bin Laden na kwamba mwili wake umetupwa baharini.

Usama bin Laden

Kwa upande wake Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa hauwezi kuthibitisha habari iliyotangazwa na maafisa wa serikali ya Marekani ya kuuawa kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr al Baghdadi.

Vilevile Wizara ya Ulinzi ya Russia imetoa taarifa ikitilia shaka habari ya mauaji ya al Baghdadi. 

Kundi la kigaidi la Daesh miaka ya hivi karibuni lilivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya nchi za Iraq na Syria likisaidiwa na Marekani, Saudi Arabia, utawala wa Kizayuni wa Israel na washirika wao na kufanya jinai za kutisha katika nchi hizo na kwengineko duniani.