Gebran Bassil: Mohammad Safadi amekubali kuwa waziri mkuu wa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i57293-gebran_bassil_mohammad_safadi_amekubali_kuwa_waziri_mkuu_wa_lebanon
Vyombo vya habari vya Lebanon vimemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje Gebran Bassil akisema kuwa waziri wa zamani wa Fedha Muhammad Safadi amekubali kuunda serikali mpya ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 15, 2019 23:15 UTC
  • Gebran Bassil: Mohammad Safadi amekubali kuwa waziri mkuu wa Lebanon

Vyombo vya habari vya Lebanon vimemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje Gebran Bassil akisema kuwa waziri wa zamani wa Fedha Muhammad Safadi amekubali kuunda serikali mpya ya nchi hiyo.

Kanali ya televisheni ya Al-Alam imeripoti kuwa, kwa mujibu wa Bassil,  suala la kuchaguliwa Mohammad Safadi, ambaye kwanza ameshawahi kushika wadhifa wa uwaziri na pia hajahusishwa kwa namna yoyote na vitendo vya ufisadi, lilijadiliwa tokea muda mrefu nyuma.

Kabla ya tangazo hilo la Gebran Bassil, baadhi ya vyombo vya habari vya Lebanon vilikuwa vimetangaza kuwa, vyama vikuu vya siasa nchini humo vimeafikiana kumpendekeza Safadi kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

Mohammad Safadi

Kabla ya kutangazwa habari hiyo, baadhi ya waandamanaji wanaopinga serikali, usiku wa kuamkia Alkhamisi walikusanyika mbele ya nyumba ya Safadi katika mji wa Tripoli kaskazini mwa Lebanon na kutoa nara za upinzani dhidi yake.

Tangu tarehe 17 Oktoba, Lebanon imekuwa ikishuhudia maandamano ya upinzani, ya wananchi wanaotaka kuboreshwa hali ya maisha na kuchukuliwa hatua kali za kupambana na ufisadi. Takribani wiki mbili tangu kuanza maandamano hayo, waziri mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri alijiuzulu wadhifa wake. 

Hata hivyo mnamo siku za karibuni, Rais Michel Aoun wa Lebanon amekuwa akitoa kauli za kuwepo matumaini ya kuundwa serikali mpya nchini humo.../