Mwendesha mashtaka wa Israel: Netanyahu alinitisha
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Utawala Haramu wa Kizayuni amesisitiza kwamba alipata vitisho vya kumtaka ajiepushe kutangaza makosa ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo.
Avichai Mandelblit, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Israel ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari ambapo amethibitisha kwamba tuhuma dhidi ya Netanyahu ni za kweli kabisa. Amezidi kufafanua kuwa tuhuma hizo zinajumuisha upokeaji rushwa, ulaghai, kusema uongo, kufanya uchakachuaji na uhaini katika amana. Ameongeza kwamba wamefanya uchunguzi zaidi na kujikinaisha kikamilifu kwamba Netanyahu amekiuka sheria za uhalifu za utawala wa Israel. Aidha sambamba na kuashiria kuwa alikabiliwa na vitisho na mashinikizo kutoka kwa waziri huyo mkuu wa Israel, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni amesema kuwa uchunguzi haukuingiliwa na masuala ya kisiasa.
Hii ni katika hali ambayo, baada ya kutangazwa tuhuma dhidi yake, Netanyahu bila kupoteza muda ameelekeza tuhuma zinazomkabili kwa vyombo vya mahkama, polisi na asasi nyingine za utawala wa Kizayuni kwamba zimekula njama katika kubuni tuhuma alizozitaja kuwa ni bandia na za kisiasa dhidi yake. Aidha amedai kwamba tuhuma zilizotangazwa dhidi yake ni hatua za kuelekea mapinduzi ya kijeshi ya kuiondoa madarakani serikali ya mrengo wa kulia. Waziri mkuu huyo wa utawala pandikizi wa Kizayuni amesisitiza kwamba kamwe hatojiuzulu madarakani.