Syria yazidi kukomboa maeneo yaliyotekwa na magaidi wakufurishaji
Jeshi la Syria limezidi kukomboa maeneo yaliyokuwa yametekwa na magenge ya kigaidi huko kusini mashariki mwa mkoa wa Idlib yakiwemo maeneo ya Umm Halahil na Dahraz-Zarzur.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, jeshi la Syria limefanikiwa kukomboa maeneo manne muhimu katika kipindi cha siku nne zilizopita.
Nalo shirika la habari la Sputnik limeripoti habari hiyo na kusema kuwa baadhi ya maeneo hayo yalikombolewa Jumapili usiku na mengine jana Jumatatu kutoka kwenye makucha ya magenge ya kigaidi ya Jabhatunnusra na Ajnad al-Kavkaz.
Kwa mujibu wa habari hiyo, jeshi la Syria limeyasababishia hasara kubwa magenge hayo ya wakufurishaji yanayoungwa mkono na madola ajinabi. Maeneo mengine muhimu yaliyokombolewa na jeshi la Syria kutoka mikononi mwa magenge hayo ya kigaidi ni Sir na al Musharrafah liliko kusini mashariki mwa mkoa wa Idlib na kufanikiwa kudhibiti kikamilifu maeneo yake ya kilimo.
Tarehe 16 mwezi huu wa Novemba, jeshi la Syria lilianza awamu ya pili ya operesheni zake za kuwafurusha magaidi kwenye mkoa wa Idlib. Awamu hiyo ilianza kwa mashambulizi makubwa ya anga na mizinga. Mkoa wa Idlib ndiyo ngome ya mwisho iliyoko mikononi mwa magenge ya kigaidi na iwapo utakombolewa kikamilifu, tutaweza kusema kuwa magaidi wameangamizwa kikamilifu nchini Syria.
Jeshi la Syria limekuwa likipata mafanikio mtawalia katika vita vyake dhidi ya magaidi. Miongoni mwa mafanikio makubwa ni jeshi hilo kukomboa mji wa kiistratijia wa Khan Sheikhoun na kudhibiti barabara kuu ya kimataifa ya Damascus-Aleppo.