Baada ya vuta nikuvute hatimaye Lebanon yapata Waziri Mkuu
Baada ya vuta nikuvute ya kisiasa nchini Lebanon, hatimaye nchi hiyo imefanikiwa kupata Waziri Mkuu mpya ikiwa ni karibu miezi miwili tangu alipojiuzulu Saad Hariri aliyekuwa akishikilia wadhifa huo.
Hassan Diab shakhsia wa kisiasa ambaye amechaguliwa miongoni mwa Waislamu wa Kisuni jana alifanikiwa kupata kura 69 za Wabunge na hivyo kupasishwa rasmi kuwa Waziri Mkuu mpya wa Lebanon.
Hassan Diab anayemrithi Saad Hariri ana muda wa majuma mawili hadi matatu awe ameunda baraza jipya la mawaziri na hivyo kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro na mkwamo wa uongozi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa wadhifa huo, Waziri Mkuu mpya wa Lebanon amesema kuwa, uthabiti wa kisiasa, kiuchumi, usalama wa kijamii, utawala wa sheria na umoja wa kitaifa ndio hitajio la nchi hiyo.
Hassan Diab ambaye amewahi kuwa Waziri wa Elimu wa Lebanon kati ya 2011 na 2014 sambamba na kubainisha kwamba, kwa sasa Lebanon inakabiliwa na mgogoro wa kitaifa amesisitiza kuwa, hivi sasa siyo wakati wa mzozo wa kisiasa na kutanguliza maslahi binafsi.
Kadhalika ameeleza kwamba, utulivu na umoja ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele na watu wote kwa ajili ya kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa sasa.
Tangu tarehe 17 Oktoba, Lebanon imekuwa ikishuhudia maandamano ya upinzani, ya wananchi wanaotaka kuboreshwa hali ya maisha na kuchukuliwa hatua kali za kupambana na ufisadi. Takribani wiki mbili tangu kuanza maandamano hayo, aliyekuuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri alijiuzulu wadhifa wake na kuifanya nchi hiyo kkuingia katika mkwamo mwingine wa uongozi.