Netanyahu apongeza juhudi za Imarati za kuimarisha uhusiano na Israel
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amepongeza jitihada zinazofanywa na Umoja wa Falme za Kiarabu za kutaka kuimarisha na kufanya wa kawaida uhusiano wa utawala huo pandikizi na baadhi ya nchi za Kiarabu.
Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Benjamin Netanyahu amesema, "Ninakaribisha uhusiano wa karibu kati ya Israel na nchi nyingi za Kiarabu. Wakati umefika kuufanya wa kawaida uhusiano huo."
Kauli hiyo ya Netanyahu imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati, kuunga mkono na kusambaza makala kwenye ukurasa wake wa Twitter inayoshabikia mpango wa kuunda muungano wa pamoja wa Waarabu na Israel.
Sheikh Abdullah bin Zayed bin Sultan Aal Nahyan amesambaza makala iliyochapishwa kwenye jarida la kila wiki la Uingereza la The Spectator, iliyoandikwa chini ya anwani inayosema: Mageuzi ya Uislamu; Muungano wa Israel na Waarabu unastawi Mashariki ya Kati.
Makala hiyo mbali na kuashiria kuhusu safari ya Netanyahu nchini Oman Oktoba mwaka jana imedai kuwa, moja ya mambo yaliyochangia kuimarika uhusiano kati ya Tel Aviv na nchi nyingi za Kiarabu, ni makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015, kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi kubwa duniani.
Nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel zimekuwa zikiyaponda makubaliano hayo hata kabla ya kuafikiwa kwake, jambo lililopelekea Rais wa Marekani, Donald Trump achukue hatua ya upande mmoja na iliyo kinyume cha sheria ya kujiondoa kwayo.