Hizbullah ya Lebanon: Tutaiunga mkono serikali mpya
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbulla ya Lebanon amesema kuwa harakati hiyo itaonyesha imani yake kwa serikali mpya ya nchi hiyo kwa kuwa ina shakhsia wanaofaa.
Sheikh Naim Qassem amebainisha kwamba migogoro ambayo imekuwa ikishuhudiwa kwa kipindi cha miaka 30 iliyopita nchini Lebanon, hii leo imefikia kwenye kiwango cha kulipuka hivyo ni suala lisilowezekana kutatuliwa katika kipindi cha siku chache au wiki chache na badala yake ni lazima kuipa fursa serikali ya Hassan Diab ijaribu kutatua matatizo ya hivi sasa ya nchi hiyo. Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ameitaka serikali mpya kuandaa na kupitisha mipango na miradi ambayo itasaidia kuboresha hali ya kifedha, kiuchumi na kijamii ya Lebanon.
Sheikh Naim Qassem ameendelea kubainisha kuwa muqawama umeweza kufikia malengo makubwa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kukiwemo kuushinda utawala haramu wa Kizayuni na kuwatimua Wazayuni kutoka ardhi za Lebanon sambamba na kushina vita vingi na utawala huo khabithi. Kadhalika sambamba na kulaani mpango wa Kimarekani wa Muamala wa Karne amesema kuwa mpango huo umezaliwa ukiwa tayari umefariki dunia kama ambavyo hauwezi kufufuka. Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, kukabiliana na mpango huo pamoja na taathira zake hasi katika ngazi ya kiutamaduani na kifikra kutategemea muqawama na kusimama imara.