Kuundwa serikali mpya ya Lebanon; mafanikio na changamoto
Bunge la Lebanon siku ya Jumanne liliidhinisha baraza jipya la mawaziri la nchi hiyo ambalo lilipendekezwa na Waziri Mkuu Hassan Diab. Baraza hilo lilipitishwa kwa kura 63 za 'ndio' na 20 za 'la' huku mbunge mmoja akijizuia kupiga kura katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wabunge 84 kati ya wabunge wote 128 wa Bunge la Lebanon.
Kuundwa baraza jipya la mawaziri nchini Lebanon ni mafanikio muhimu katika muundo wa nguvu za kisiasa na makundi ambayo yanamuunga mkono waziri mkuu mpya wa nchi hii kwa sababu pamoja na kuwapo changamoto na uvurugaji wa ndani na nje ya nchi, hatimaye baraza la mawaziri limeundwa.
Harakati ya Kitaifa ya Uhuru inayoongozwa na Gebran Bassil, Harakati ya Kishia ya Amal inayoongozwa na Nabih Berri, Chama cha Marada kinachoongozwa na Suleiman Frangieh na Mrengo wa Muqawama unaofungamana na Harakati ya Hizbullah pamoja na mirengo kadhaa ya Ahul Sunna ni kati ya waungaji mkono wa serikali mpya ya Lebanon.
Katika upande wa pili Harakati ya Al Mustaqbal inayoongozwa na Saad Hariri, Chama cha 'Vikosi vya Lebanon' kinachoongozwa na Samir Geagea na Chama cha Kisochialisti kinachoongozwa na Walid Jumblatt ni kati ya wapinzani wakuu wa serikali mpya ya waziri mkuu Hassan Diab.
Muundo wa waungaji mkono na wapinzani wa serikali mpya unaonyesha kuwa, serikali hii imeundwa kwa uungaji mkono wa upande wa waliowengi katika bunge yaani Mrengo wa Machi 8 na waitifaki wake ambao wako karibu na Harakati ya Hizbullah. Katika upande wa pili, serikali ya Diab pia ina wapinzani sugu ambao wanaweza kuvuruga utendaji kazi wake.
Kuhusiana na nukta hii waungaji mkono wa mrengo huu, siku ya Jumanne usiku walifanya maandamano na kuibua ghasia kwa lengo la kubainisha upinzani wao kwa serikali mpya.
Aidha kuundwa serikali inayoongozwa na Hassan Diab kuna maana ya kufika ukingoni zama za utawala wa ukoo wa Hariri katika muundo wa kisiasa wa Lebanon. Saad Hariri na baba yake, hayati Rafiq Hariri, wamekuwa madarakani Lebanon aghalabu ya muda wote wa miongo mitatu iliyopita. Kuundwa serikali mpya kunaonyesha kuwa ule mchezo wa kisiasa wa kujiuzulu ili kupata manufaa, ambao umekuwa ukichezwa na Saada Hariri, umegonga mwamba.
Kwa muda mrefu Hariri amekuwa akidhani kuwa, katika jamii ya Ahul Sunna, ambayo imetengewa kiti cha uwaziri mkuu katika muundo wa kisiasa Lebanon, hakuna mtu mwingine anayeweza kushika nafasi ya waziri mkuu isipokuwa yeye. Kwa msingi huo, siku 13 tu baada ya kuanza maandamano ya wananchi, Hariri alijiuzulu kwa lengo la kuanza mazungumzo ya kuwalazimisha mahasimu wake walegeze misimamo kabla ya kuundwa serikali mpya. Hata hivyo mbinu hiyo iliambulia patubu baada ya Diab kuunda serikali mpya na hivyo kubadilisha mlingano wa kisiasa nchini Lebanon.
Mbali na changamoto za kisiasa, baraza jipya linakabiliwa na changamoto muhimu za kiuchumi. Kupungua mishara na uwezo wa wafanyakazi kununua bidhaa za kila siku maishani, ongezeko la ushuru, nakisi kubwa ya bajeti, kupungua thamani ya sarafu ya kitaifa, kusimamishwa uingizwaji wa sarafu ya dola Lebanon, kukimbia wawekezaji na wasomi, madeni makubwa ya kigeni na pia ufisadi mkubwa wa kiuchumi ni kati ya changamoto muhimu zaidi za kiuchumi zinazoikabili serikali hiyo mpya.
Hassan Diab anasema kumalizwa matitizo hayo ya kiuchumi na kimaisha ni kipaumbele muhimu kwa serikali yake kwani matatizo hayo ndio chanzo cha maadanamano ya wananchi dhidi ya serikali. Diab anafafanua zaidi kuhusu nukta hii kwa kusema: "Baraza la Mawaziri la Lebanon, ili kutekeleza matakwa ya wananchi, litatumia mfumo huru wa mahakama ili kurejesha mali zilizoporwa na kukabiliana na utajiri uliopatikana kwa njia haramu sambamba na kuwaunga mkono watu masikini katika jamii ambao wanakabiliwa na mfumo dhalimu wa kodi na ushuru. Aidha amesema serikali yake pia itazingatia kwa kina suala la kukabiliana na ukosefu wa ajira na pia kuhakikisha kuwa kunapitishwa sheria mpya za uchaguzi.