"Marekani ilivuka mistari yote miekundu kwa kumuua shahidi Jen. Soleimani"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59139-marekani_ilivuka_mistari_yote_miekundu_kwa_kumuua_shahidi_jen._soleimani
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kwa kumuua kigaidi shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Qods cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ( SEPAH), Marekani ilivuka mistari yote miekundu na kwamba mauaji hayo yamegeuza mahesabu yote katika eneo la Asia Magharibi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 14, 2020 03:24 UTC

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kwa kumuua kigaidi shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani Kamanda wa Kikosi cha Qods cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ( SEPAH), Marekani ilivuka mistari yote miekundu na kwamba mauaji hayo yamegeuza mahesabu yote katika eneo la Asia Magharibi.

Sayyid Hassan Nasrullah amesema hayo jana usiku kwa njia ya televisheni kutoka Beirut, mji mkuu wa Lebanon kwa mnasaba wa arubaini ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani na wanajihadi wenzake na kuongeza kuwa, jinai hiyo ya Washington imepelekea kufunguliwa ukurasa mpya wa historia katika eneo la Asia Magharibi.

Ameeleza bayana kuwa, "mauaji ya kamanda wa ngazi za juu wa Iran yameusaidia umma wa Kiislamu kutambua adui yao mkubwa, ambaye ni shetani mkubwa Marekani."

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, sababu kuu ya Marekani kutekeleza mauaji hayo ya kigaidi ni kugonga mwamba malengo yake machafu katika eneo na kwamba, licha ya ugaidi huo lakini athari za Jenerali Soleimani hivi sasa zimeonekana na kuhisika zaidi kieneo na kimataifa kuliko wakati wowote ule.

Marasimu ya arubaini ya Soleimani na Mashahidi wenzake yamefanyika kote Iran

Kamanda Qassem Soleimani ambaye Januari 3 mwaka huu alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la wanajeshi magaidi wa Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.  

Marasimu ya arubaini ya Kamanda Soleimani na wanajihadi wenzake yalifanyika jana usiku hapa Tehran kwa kuhudhuriwa na wananchi Waislamu wa Iran na wageni kutoka nje ya nchi.