Radiamali ya Sayyid Hassan Nasrullah kuhusu kadhia ya Amer Al-Fakhoury
Kuachiliwa huru na kutoroshwa Amer Al-Fakhoury, kibaraka mwenye uraiapacha wa Lebanon na Marekani, ilikuwa ndio maudhui kuu ya hotuba aliyotoa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon usiku wa kuamkia jana.
Itakumbukwa kuwa wakati utawala haramu wa Kizayuni ulipolivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la kusini mwa Lebanon, Amer Al-Fakhoury alikuwa mwanachama wa kundi moja la vibaraka wa utawala huo, lililokuwa linaitwa 'Jeshi la Kusini ya Lebanon'; na alikuwa mhusika mkuu wa utesaji wa wafungwa Walebanon waliokuwa wakishikiliwa katika mahabusu ya Al-Khayyam, kusini mwa nchi hiyo. Septemba iliyopita na baada ya kuishi miaka 20 nchini Marekani Al-Fakhoury, alirejea Lebanon na akatiwa mbaroni kwa amri ya mahkama ya kijeshi ya nchi hiyo kwa tuhuma za kuwatesa wafungwa wa mahabusu ya Al-Khayam. Kwa kipindi cha miezi 6 akiwa kizuizini Lebanon, serikali ya Marekani ilitumia njia tofauti kuishinikiza Lebanon ili imwachie huru Al-Fakhoury. Katika hotuba yake, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah alizungumzia suala hilo na kubainisha kuwa, Wamarekani waliwatishia moja kwa moja baadhi ya shakhsia wa kisiasa na serikali ya Lebanon kwamba iwapo hawatomfutia tuhuma na kumuachilia huru Amer Al-Fakhoury, basi itawawekea vikwazo.
Mashinikizo ya serikali ya Marekani dhidi ya Lebanon ya kutaka kuachiliwa huru Al-Fakhoury yalijiri katika hali ambayo mwaka 1998 na kabla ya kutoroka nchi hiyo ya Kiarabu, mamluki huyo alihukumiwa na vyombo vya mahkama vya nchi hiyo bila kuwepo mahakamani kifungo cha miaka 15 jela kwa tuhuma za kuwa kibaraka wa Wazayuni. Ukweli ni kwamba wakati Amer Al-Fakhoury aliporejea nchini Lebanon mwezi Septemba 2019, hakutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela kinachotokana na tuhuma za kuwa kibaraka wa utawala haramu wa Kizayuni. Hatimaye wiki iliyopita ya tarehe 16 Machi mahkama ya kijeshi ya Lebanon na baada ya miezi sita, ilikubali utetezi uliowasilishwa na wakili wa Al-Fakhoury, kwa kisingizio cha tuhuma zilizopitwa na wakati zinazomkabili mteja wake na hivyo ikatoa hukumu ya kuachiliwa kwake huru kwa sharti kwamba asitoke nje ya ardhi ya Lebanon. Pamoja na hayo Wamarekani hawakukubali mtuhumiwa huyo kuachiliwa huru kisha aendelee kubakia nchini humo ambapo wiki iliyopita walimtorosha kutoka Lebanon, suala ambalo lilithibitishwa hata na Rais Donald Trump Alkhamisi iliyopita wakati akizungumza na waandishi wa habari. Akizungumzia suala hilo Trump alisema: "Tulilipa umuhimu suala la kuachiliwa Amer Al-Fakhoury mwenye uraia wa Lebanon na Marekani." Hatua hii ya Marekani imelalamikiwa vikali na wananchi, makundi ya kisiasa na Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi ya Hizbullah ya Lebanon. Katika uwanja huo raia wa Lebanon walikusanyika mbele ya mahkama ya kijeshi huku baadhi yao wakichoma moto matairi ya magari na kufunga baadhi ya barabara kuu za nchi hiyo.
Nukta muhimu ni hii kwamba, baadhi ya mirengo ya ndani na nje ya Lebanon na baada ya kukubaliana na Marekani, ilifanya njama za kujaribu kuzitwisha dhima ya kuachiliwa huru kibaraka huyo Harakati ya Hizbullah na Mrengo wa 'Matumaini ya Lebanon.' Hii ni katika hali ambayo, suala hilo kwa upande mmoja linapingana kiujumla na misingi ya kifikra na itikadi ya Hizbullah kwa kuwa harakati hiyo haina mahusiano hata kidogo na Marekani kama ambavyo inapinga vikali uwepo wa Washington katika eneo, na kwa upande mwingine inapinga uingiliaji wa Washington katika masuala ya ndani ya Lebanon. Aidha kwa upande mwingine Sayyid Hassan Nasrullah alibainisha kwamba Harakati ya Hizbullah si tu kwamba haikuhusika kwa namna yoyote katika kuachiliwa huru Amer Al-Fakhoury, bali hata yenyewe ilipata habari za kuachiliwa huru mtuhumiwa huyo kupitia vyombo vya habari. Akikosoa uamuzi wa kamati ya mahkama ya kijeshi ya Lebanon katika kutoa hukumu ya kuachiliwa huru Al-Fakhoury alisisitiza kuwa: "Uamuzi wa kuachiliwa huru kibaraka huyo haukuchunguzwa na serikali na wala uamuzi kama huo haukuchukuliwa na serikali yote ya Lebanon." Ukweli ni kwamba wapinzani, ambao hapo kabla walishindwa kuunda serikali itakayoendana na matakwa yao, baada ya kuteuliwa waziri mkuu mpya na kuundwa serikali, hivi sasa wanafanya njama za kuitumia kadhia ya kuachiliwa huru kibaraka Al-Fakhoury ili kuikosoa serikali ya Hassan Diab, Harakati ya Hizbullah na Mrengo wa Matumaini na kwa njia hiyo kuchochea fikra za waliowengi ili kuibua tena ghasia na machafuko kupitia maandamano ya barabarani nchini humo.