Adnan al Zurfi aunga mkono harakati ya al Hashd al Sha'abi
Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Iraq ameiunga mkono harakati ya kujitolea ya wananchi wa Iraq ya al Hashd al Sha'abi.
Adnan al Zurfi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Harakati ya al Hashd al Sha'abi ni taasisi ya kijeshi ya Iraq iliyoundwa kwa mujibu wa sheria za bunge na matakwa ya wananchi kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kuikomboa Iraq.
Al Zurfi ameongeza kuwa Harakati ya al Hashd al Sha'abi itaendelea kuwa harakati imara na tiifu kwa Iraq na kwa Wairaqi. Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Iraq amebainisha kuwa iwapo atafanikiwa kuunda serikali, ajenda yake kuu na siasa zake za nje zitajikita katika suala la kudumisha uhusiano wa kirafiki na nchi jirani, nchi za eneo na jamii ya kimataifa sambamba na kulinda maslahi, mamlaka na kujitawala Iraq.
Adnan al Zurfi alipewa jukumu la kuunda serikali ya mpito huko Iraq kufuatia dikri iliyotolewa Machi 17 mwaka huu na rais wa nchi hiyo Barhum Salih. Kuchaguliwa al Zurfi kushikilia wadhifa huo kumepingwa na kulalamikiwa na makundi ya Kishia nchini humo.