Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala haramu wa Kizayuni awekwa karantini
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Utawala Haramu wa Kizayuni wa Israel imetangaza kuwa, Benjamin Netanyahu na wasaidizi wake kadhaa, wamewekwa karantini ya nyumbani.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu huyo wa utawala bandia wa Kizayuni imeongeza kuwa, kupatikana na maambukizi ya Corona Rivka Paluch, msaidizi wa karibu wa Benjamin Netanyahu, kumempelekea Netanyahu na wasaidizi wake wengine kuwekwa karantini ya nyumbani. Jumapili iliyopita gazeti la Times of Israel liliandika habari ya kuathirika Rivka Paluch, baada ya kupimwima na kubainika kuwa na virusi vya Corona. Kwa mujibu wa habari hiyo, baada ya msaidizi huyo wa karibu wa Netanyahu kukutwa na maambukizi hayo, mke wake pia alilazimika kufanyiwa vipimo.
Wizara ya Afya ya Utawala wa Kizayuni pia imetangaza kuwa, idadi ya waathirika wa virusi vya Corona ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu imefikia 4,347. Wakati huo huo Baraza la Mawaziri la Israel limepasisha sheria ya kupiga marufuku mikusanyiko ya zaidi ya watu 10 na pia kuchunga masafa ya mita mbili baina ya mtu na mtu. Aidha siku chache zilizopita, Netanyahu alitangaza kwamba, kuna uwezekano wa watu milioni moja wakaambukizwa virusi hivyo huko Israel.