Madai ya kushangaza ya Saudia; serikali ya Mansur Hadi inaihudumia Iran
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60421-madai_ya_kushangaza_ya_saudia_serikali_ya_mansur_hadi_inaihudumia_iran
Siku ya Jumatano Muhammad Aal Jabir, balozi wa Saudi Arabia nchini Yemen alimtuhumu Ahmed Saleh Al-Issa, naibu mkuu wa masuala ya kiuchumi wa ofisi ya Abdurabbuh Mansur Hadi, rais aliyestaafu na kukimbia nchi wa Yemen kuwa anaiuzia mafuta Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2020 02:34 UTC
  • Madai ya kushangaza ya Saudia; serikali ya Mansur Hadi inaihudumia Iran

Siku ya Jumatano Muhammad Aal Jabir, balozi wa Saudi Arabia nchini Yemen alimtuhumu Ahmed Saleh Al-Issa, naibu mkuu wa masuala ya kiuchumi wa ofisi ya Abdurabbuh Mansur Hadi, rais aliyestaafu na kukimbia nchi wa Yemen kuwa anaiuzia mafuta Iran.

Ni wazi kuwa Saudia imekwama katika kinamasi cha Yemen. Moja ya sababu kuu za Saudia kuanzisha vita dhidi ya Yemen ni kwamba ilidai kuwa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ina uhusiano mkubwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuchukua kwake madaraka ya huko Sanaa, mji mkuu wa Yemen, kungekuwa hatari kubwa kwa usalama wa kijeshi na ardhi ya Saudia.

Katika utambulisho wake, Ansarullah ni harakati ya Kishia ambayo ina mitazamo inayokinzana na ya watawala wa ukoo wa Aal Saud. Pamoja na hayo lakini harakati hiyo sio ya Kishia tu bali inajumuisha wanaharakati wa Kisuni ambao wanapinga umamizi wa Wasaudi katika ardhi yao. Watawala wa Aal Saud walikuwa wakidhani kwamba kwa kueneza propaganda hiyo chafu kupitia makundi ya kimadhehebu, wangeweza kuwachochea Wayemen wasimame dhidi ya Ansarullah, lakini ilibainika wazi kuwa walikosea sana katika uchochezi wao huo kwa sababu hata jeshi lililokuwa chini ya serikali ya wakati huo ya Ali Abdallah Swaleh pia ilikuwa ikishirikiana kwa karibu na harakati hiyo ya Kiislamu.

Muhammad bin Salman aliyefedheheshwa katika vita vyake vya kichokozi Yemen

Kushindwa Saudi Arabia kuiangusha Ansarullah katika vita vya Yemen wakati mmoja kuliwafanya watawala wa Riyadh waanze kutafuta visingizio vya kushindwa huko na hivyo kudai kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa inawasaidia wanaharakati hao kwa makombora na suhula nyingine za kijeshi. Walipata uungaji mkono wa Marekani kuhusu madai hayo ambapo hata Nikki Haley, balozi wa wakati huo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, mwezi Disemba 2017 alionyesha kitu kilichofanana na chuma kubwa  na kudai kuwa yalikuwa mabaki ya kombora lililolipuliwa la Iran.

Saudia pia iliakisi madai hayo ya Haley kwa kuonyesha mjini Makka mwezi Mei 2019 mabaki yaliyodaiwa kuwa ya kombora la Iran. Wakati huo ilikuwa mwenyeji wa vikao vitatu muhimu vya viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Umoja wa Ushirikiano wa Nchi za Kiislami. Ilidai kwamba silaha zilizoonyeshwa kwenye sarakasi hiyo ya kuchekesha ndizo zilezile zinazotolewa na Iran kwa Ansarullah ya Yemen. Saudia ilichukua hatua hiyo ili kuidogosha Ansarullah na wakati huohuo kujaribu kuonyesha kuwa kichapo kikali ilichopata kutoka kwa Ansarullah hakingewezekana isipokuwa kutoka kwa nchi yenye nguvu kama Iran, ili kwa njia hiyo isiweze kudhalilika mbele ya fikra za waliowengi duniani. Kudumishwa ushindi wa Ansarullah hasa kuhusiana na suala la mashambulio ya makombora na droni za jeshi na kamati za wananchi wa Yemen dhidi ya Saudia, hadi umbali wa kilomita 1200 ndani ya ardhi ya nchi hiyo, kumethibitisha kwamba madai yanayotolewa na utawala huo dhidi ya Iran hayana ukweli wowote.

Nikki Haley akitoa madai bandia dhidi ya Iran mbele ya waandishi wa habari mjini New York

Hivi sasa Saudia imeanzisha madai mengine dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kudai kuwa ina uhusiano na ofisi ya rais wa serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi. Madai hayo na mengine kama vile ya Iran kuuziwa mafuta yake na ofisi ya serikali hiyo iliyojiuzulu yanatolewa katika hali ambayo kumejitokeza hitilafui kubwa kati ya utawala wa Riyadh na baadhi ya wanachama wa serikali hiyo iliyojiuzulu. Hitilafu hizo ziliongezeka hasa baada ya serikali hiyo ya Mansur Hadi kushindwa kukabiliana na Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen ambalo linafungamana na Imarati, katika majira ya joto kali mwaka uliopita, ambapo hata baadhi ya wanachama wa serikali hiyo walianza kuukosoa waziwazi utawala wa Saudia.

Hivi sasa kwa kuanzisha tuhuma zisizo na msingi dhidi ya maafisa wa ofisi ya Mansur Hadi na kuzihusisha na Iran, watawala wa Riyadh wanafanya juhudi za kufunika aibu ya kushindwa kwao na jeshi pamoja na kamati za wananchi wa Yemen katika medani ya vita na wakati huohuo kujaribu kuonyesha kuwa sababu ya kuongezeka hitilafu kati yao na serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi, ni usaliti unaofanywa na maafisa wachache wa serikali ya rais huyo wa zamani wa Yemen, ambaye ni kibaraka mkubwa wa ukoo wa Aal Saud.