Wapalestina wakusanyika Nablus, Ufukwe wa Magharibi kupinga safari ya Pompeo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60992-wapalestina_wakusanyika_nablus_ufukwe_wa_magharibi_kupinga_safari_ya_pompeo
Wananchi wa Palestina wamekusanyika katika mji wa Nablus ulioko kaskazini mwa Ufukwe wa Magharibu wa Mto Jordan kupinga safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la 'Israel'.
(last modified 2026-05-06T11:35:21+00:00 )
May 15, 2020 03:40 UTC
  • Wapalestina wakusanyika Nablus, Ufukwe wa Magharibi kupinga safari ya Pompeo

Wananchi wa Palestina wamekusanyika katika mji wa Nablus ulioko kaskazini mwa Ufukwe wa Magharibu wa Mto Jordan kupinga safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la 'Israel'.

Siku ya Jumatano, Pompeo alielekea Israel ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala huo haramu wa Kizayuni.

Ripoti kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu zinasema, Wapalestina kadhaa jana walikusanyika mjini Nablus kupinga na kulaani safari ya Mike Pompeo katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu wakisisitiza kuendeleza upinzani pia dhidi ya mpango wa Kimarekani na Kizayuni wa 'Muamala wa Karne' na sera za serikali ya Marekani kuhusiana na taifa madhulumu la Palestina.

Kutoka kushoto: Pompeo, Netanyahu na Trump

Wapalestina hao waliokuwa wakipaza sauti zao kulaani sera za Marekani za kuupendelea utawala wa Kizayuni, wamesema, safari ya Pompeo inamaanisha kuunga mkono mpango wa Israel wa kunyakua baadhi ya maeneo ya Ufukwe wa Magharibi na kuyaunganisha na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la 'Israel'.

Utawala wa Kizayuni umepanga ifikapo mwezi Julai mwaka huu, uanze kutekeleza mpango wa kuyaunganisha baadhi ya maeneo ya eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu.../