Kufichuliwa kashfa ya Saudia ya kutuma maelfu ya magaidi nchini Iraq
Kusambazwa faili la sauti katika mitandao ya kijamii kumepelekea kufichuliwa kashfa ya Saudi Arabia kutuma maelfu ya magaidi wa nchi hiyo kwenda Iraq katika miaka ya hivi karibuni.
Kashfa hiyo inahusu mahojiano ya simu kati ya Kanali Muammar al-Gaddafi, kiongozi wa zamani wa Libya na Yusuf bin Alawi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman ambapo Bin Alawi anaelezea habari ya kutumwa na Saudia magaidi 4000 kwenda Iraq. Katika mazungumzo hayo ambayo yanahusiana na miaka ya tokea 2004 hadi 2007, Kanali Muammar al-Gaddafi alimwambia Yusuf bin Alawi kwamba Marekani inafanya juhudi za kuumaliza utawala wa Aal-Saud. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa zamani wa Libya, Wamarekani waliamini kwamba muda wa itibari wa utawala wa Saudi Arabia ulikuwa umepita na kwamba walikuwa wanafuatilia mbadala wa watawala wa Aal-Saud, kwa sababu watawala hao walikuwa hatari kwa Marekani na usalama wa eneo la Asia Magharibi.
Baada ya kufichuliwa na kusambaa faili hilo la sauti, watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Iraq wametuma jumbe wakitaka kukabiliana na hatua za Riyadh katika kueneza ugaidi. Abu Ali Al-Askari, Msemaji na Kamanda wa Kundi la Hizbullah ya Iraq ametaka kutolewa jibu kali dhidi ya Saudia. Naye Nasr Al-Shimri, Msemaji wa Kundi la Muqawama wa Kiislamu la Al-Nujaba nchini Iraq ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya magaidi 4000 wakipewa taarifa na uungaji mkono kutoka kwa utawala wa ukufurishaji na wa Kiwahabi wa Aal-Saud waliingia Iraq.