Kubaidishwa khatibu wa Msikiti wa al Aqsa; jinai mpya ya Wazayuni
Polisi ya utawala wa Kizayuni imetoa amri ya kubaidishwa kwa miezi minne Sheikh Ikrima Sabri Khatibu wa Msikiti wa al Aqsa.
Sheikh Ikrima Sabri alitiwa mbaroni na wanajeshi wa Israel nyumbani kwake siku ya Ijumaa na kulazimishwa kuwa mbali na Msikiti wa al Aqsa kwa muda wa wiki moja. Vitendo vya mabavu vya Wazayuni dhidi ya Sheikh Sabri vinahusiana na msimamo wake kuhusu Msikiti wa al Aqsa. Sheikh Sabri anafahamu vyema kuwa Msikiti wa al Aqsa ni kibla cha kwanza cha Waislamu na amelaani vikali hatua ya utawala wa Kizayuni ya kujaribu kuuyahudisha msikiti huo mtakatifu. Utawala wa Kizayuni unamtuhumu Sheikh Sabri kwa kufanya uchochezi na kudai kuwa matamshi yake yanawachochea wananchi wa Palestina dhidi ya Israel.
Madai haya ya utawala wa Kizayuni yaliyosababisha kutolewa tuhuma bandia na kuchukuliwa hatua dhidi ya Sheikh Ikrina Sabri yametolewa katika hali ambayo Msikti wa al Aqsa ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Wapalestina kiasi kwamba Intifadha ya al Aqsa ilianza mwaka 2000 kutokana na taathira za Wazayuni kuuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa.
Utawala unaoikalia Quds kwa mabavu unafanya jitihada za kuuyahudisha Msikiti wa al Aqsa ili kuwapokonya Wapalestina utambulisho wao wa kidini na kukamilisha kuzikalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina. Ukweli wa mambo ni kuwa utawala wa Kizayuni unatoa madai ya kuwa na mamlaka kwa msikiti mtakatifu wa al Aqsa; na vitendo vyake kama vile kumbaidisha kwa miezi minne Sheikh Sabri pia vinajiri katika mkondo huo. Nukta nyingine ni hii kuwa utawala wa Kizayuni unafanya kila unaloweza kutekeleza hatua iliyo kinyume cha sheria ya kuyaunganisha na ardhi unazozikalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuanzia kuanzia Julai Mosi. Vitendo vya ukatili na tuhuma kama zile zilizoelekezwa kwa Sheikh Ikrima Sabri zinanatolewa kwa lengo la kuzusha hofu na wahaka dhidi ya shakhsia wa kisiasa na kidini wa Palestina; ili kuzuia malalamiko na maandamano ya Wapalestina na hivyo kuuwezesha utawala huo kusogeza mbele mpango wake haramu wa kuziunganisha ardhi za Wapalestina na zile unazozikalia kwa mabavu.
Kuhusiana na suala hilo Sheikh Sabri ametoa radiamali yake kwa amri hiyo ya Israel kwa kusema: Hii ni taswira halisi ya maghasibu ambao wanafanya juhudi za kutunyamazisha huku wao wakiughusubu Msikiti wa al Aqsa kinyume cha sheria. Kadhia nyingine ni kuwa, kitendo cha utawala wa Israel cha kumbaidisha kwa miezi minne Khatibu wa Msikiti wa al Aqsa kwa mara nyingine tena kinaonyesha kupuuzwa indhari za kimataifa kuhusu madhara na taathira za vitendo haramu vinavyotekelezwa na Israel dhidi ya raia wa Palestina. Katika siku za karibuni viongozi wa nchi mbalimbali na pia Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya walitahadharisha mara kadhaa kuhusu taathira hasi za kuyaunganisha baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu; na kutaka kusitishwa mipango ya kujitanua na kughusubu ardhi za Palestina ya utawala wa Kizayuni.
Josep Borrell Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya hivi karibuni alieleza kuwa: Sisi tunaitaka Israel iachane na uamuzi wowote wa upande mmoja utakaopelekea kuunganishwa ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na kukiukwa sheria za kimataifa. Nukta ya mwisho ni kwamba hatua ya kinyume cha sheria ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Sheikh Ikrima Sabri inatekelezwa katika kivuli cha kutoelewana, hitilafu na migawanyiko katika Ulimwengu wa Kiarabu na jitihada za baadhi ya nchi za Kiarabu zinazodai kuhuisha uhusiano wazo na utawala wa Kizayuni. Sheikh Ikrima Sabri Khatibu wa msikiti wa al Aqsa amesema kuhusu suala hilo kwamba: Kwa bahati mbaya juhudi zilizoanzishwa na baadhi ya nchi za Kiarabu kwa ajili ya kuhuisha uhusiano na maghasibu wa Kizayuni zimewapatia ujasiri na kuwachochea zaidi maghasibu hao kuchukua hatua za kichokozi na kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa.