Wanaharakati wa masuala ya kiraia watoa wito wa kususiwa Israel kimataifa
Jumuiya ya Kimataifa ya Mshikamano wa Kusini nchini Afrika Kusini imetoa wito wa kususiwa utawala haramu wa Israel katika nyanja za kimataifa.
Jumuiya hiyo ya kimataifa imewasilisha waraka uliotiwa saini na wasomi, wanasiasa, viongozi wa vyama, mashirika mbalimbali na wanasheria kutoka mabara ya Asia, Afrika na America ya Latini wakitoa wito wa kususiwa utawala ghasibu wa Israel kimataifa.
Waraka huo ambao pia umetiwa saini na wasomi na watu mashuhuri 250 wa Afrika Kusini, umelaani mpango wa Kimarekani wa "Muamala wa Karne" na kuupa jina jipya la "Wizi wa Karne".
Waraka huo umesema kuwa, mipango ya Israel ya kupora na kutwaa ardhi zaidi za Palestina ndio msingi wa mpango wa Donald Trump wa Muamala wa Karne unaokanyaga sheria zote za kimataifa ikiwemo haki ya taifa la Palestina ya kujiamulia mambo yake lenyewe.
Waraka huo umesisitiza kuwa, operesheni ya kuwafukuza Wapalestina katika ardhi na nchi yao na kupanua ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni inafanyika kwa msaada mkubwa wa Marekani.
Wakati huo huo wanaharakati wa kupigania haki za kiraia wameitaka Kamati ya Apartheid ya Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kukabiliana na njama za Israel na kulinda haki za Wapalestina.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameazimia kutwaa ardhi ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi tarehe Mosi mwezi Ujao wa Julai, suala amabalo limepingwa vikali na jamii ya kimataifa.