Deni la Saudia laongezeka kwa asilimia 375 wakati wa Bin Salman
(last modified Mon, 22 Jun 2020 07:30:41 GMT )
Jun 22, 2020 07:30 UTC
  • Deni la Saudia laongezeka kwa asilimia 375 wakati wa Bin Salman

Data za Benki ya Dunia zinaonesha kuwa deni la nje la Saudi Arabia limepanda vibaya mno tangu Mohammad bin Salman alipopewa cheo cha kurithi kiti cha ufalme wa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, takwimu rasmi za Benki ya Dunia zinaoensha kwamba, madeni ya serikali ya Saudi Arabia wakati huu wa Mohammad bin Salman yamepanda vibaya mno, na yameongezeka kwa zaidi ya dola bilioni 183.

Kwa mujibu wa data na takwimu hizo za Benki ya Dunia, kiwango cha madeni ya nje ya Saudia katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kimekuwa kikivunja rekodi ambazo hazijawahi kuvunjwa huko nyuma kiasi kwamba hadi mwishoni mwaka jana 2019, madeni ya Saudi Arabia yalikuwa yamepanda kwa takriban asilimia 375. Takwimu hizo zinaonesha kuwa, kiwango cha deni hilo kitapanda kwa zaidi ya asiliia 54 nyingine mwaka huu.

 

Ni vyema tukasema hapa kuwa, takwimu hizo zinahusiana na kabla ya kukumbwa Saudia na wimbi la kirusi cha corona ambapo ugonjwa huo umeathiri vibaya uchumi wa dunia tangu mwezi Machi mwaka huu. Vile vile takwimu hizo za kuporomoka vibaya uchumi ya Saudia na kupanda vibaya deni la nje la nchi hizo zinahusiana na kipindi cha kabla ya kuzuka mgogoro wa hivi karibuni wa mafuta na kuporomoka vibaya bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.

Ikumbukwe kuwa, mwezi Juni 2017, mfalme wa Saudi Arabia alimpokonya cheo cha urithi wa kiti cha ufalme, ndugu yake Muhammad bin Nayef na badala yake akampa cheo hicho mwanawe Muhammad bin Salman ambaye tangu alipopewa cheo hicho na baba yake anatuhumiwa kufanya mauaji mengi kama ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi, lakini zaidi jinai kubwa za kivita dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen. 

Tags