Uturuki: Saudia haina ustahiki wa kuendesha kesi ya wauaji wa Khashoggi
Mshauri wa Rais wa Uturuki amesisitiza kuwa, Saudi Arabia haina ustahiki wa kuendesha kesi za wauaji wa Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari raia wa Saudia aliyeuliwa kinyama ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki.
Fuat Oktay, mshauri wa Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amekosoa jinsi maafisa wa utawala wa Riyadh walivyoshughulikia faili la mauaji ya Khashoggi na kueleza kwamba: Waliohusika na jinai hiyo na watu waliowaunga mkono wangali wanaendelea kila leo kutenda jinai na kukiuka haki za binadamu ndani na nje ya Saudi Arabia.
Akizungumza sambamba na kuanza kesi ya maafisa wa Saudia wanaoshtakiwa katika mahakama ya Uturuki bila wenyewe kuwepo mahakamani kwa kuhusika na mauaji ya Jamal Khashoggi, ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Aal Saud, Oktay amekosoa vikali hatua ya maafisa wa Saudi Arabia ya kuwazuia maafisa husika wa serikali ya Uturuki wasiingie na kufanya uchunguzi katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Instanbul mara baada ya kuuliwa Khashoggi na kuongeza kuwa: Hatua hiyo ya maafisa wa Saudia ilikuwa fursa mwafaka iliyotumiwa na nchi hiyo kuharibu nyaraka na kufuta ushahidi wa mauaji hayo.
Mshauri wa Rais wa Uturuki amemkosoa pia Mkuu wa Mashtaka wa Saudi Arabia ambaye alifanya safari mjini Istanbul baada ya kuuliwa Khashoggi na kueleza kwamba, katika safari yake hiyo, si tu hakutoa taarifa zozote kuhusu hatima ya mwili wa Khashoggi na kuungama kwa washtakiwa wa mauaji yake, lakini badala yake mkuu huyo wa mashtaka wa Saudia alitaka apatiwe taarifa za mazungumzo ya simu aliyofanya Jamal Khashoggi pamoja na laptopu yake; tena si kwa ajili ya kuhakikisha haki na uadilifu unatendeka bali ni kwa ajili ya kuzidukua taarifa kwa manufaa wa wahalifu.
Kesi ya raia 20 wa Saudi Arabia wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya Jamal Khashoggi ilianza kusikilizwa siku ya Ijumaa iliyopita na mahakama ya Caglayan iliyoko mjini Istanbul, Uturuki bila washtakiwa wenyewe kuwepo mahakamani. Waendesha mashtaka wa Uturuki wamesema wameshatoa waranti wa kukamatwa washtakiwa hao.../