Saudia yakosolewa kwa kuruhusu maonyesho ya mitindo ya kifuska Madina
Utawala wa Saudia Arabia, ambao watawala wake kwa muda mrefu wanajinadi kuwa eti ni 'wahudumu wa maeneo mawili matakatifu ya Waislamu ya Makka na Madina' umekosolewa vikali kwa kuruhusu maonyesho ya mavazi ya kifuska katika mji mtukufu wa Madina.
Tovuti ya Middle East Monitor imefichua kuwa, Ufalme wa Saudia, ambao kimsingi unaongozwa na mrithi wa ufalme Mohammad bin Salman, umeliruhusu jarida la Vogue Arabia, ambalo ni nakala ya Kiarabu ya jarida la mitindo la Vogue la Marekani, kuwaleta wanamitindo wa kimataifa kufika katika mji mtakatifu wa Madina na kupigwa picha za kifuska katika mji wa kale wa la Al Ula magharibi mwa eneo la Madina.
Katika upigaji picha za kifuska uliopewa jina la "Masaa 24 Al Ula", wanamitindo wa kike walionekana wakiwa wamevaa nguo fupi na zinazowabana kinyume kabisa na mafundisho ya Kiislamu.
Kati ya wanamitindio ambao Saudia iliwaalika katika hafla hiyo ya kifuska eneo la Madina ni pamoja na Kate Moss, Mariacarla Boscono, Candice Swanepoel, Jourdan Dunn, Amber Valletta, Xiao Wen and Alek Wek.
Upigaji picha hizo za kifuska umejiri katika eneo ambalo liko kilomita 300 kutoka mji Mtakatifu wa Madina ambao pamoja na Makka ndiko iliko misikiti miwili mitakatifu zaidi ya Waislamu duniani.