Jihadul Islami ya Palestina yalalamikia njama mpya za "Google" na "Apple"
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imekosoa vikali kitendo cha mashirika ya intaneti ya Google na Apple ya Marekani ya kuondoa neno "Palestina" katika ramani zao za dunia.
Shirika la habari la al-Quds limenukuu taarifa ya harakati hiyo ya Kiislamu ya Palestina ya leo Jumapili, ambayo imelaani vikali njama hizo mpya za Marekani na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Taarifa ya Jihadul Islamu imesema hakuna shaka kuwa njama hizo batili za kujaribu kupotosha historia na utambulisho wa Palestina na ambazo zinaunga mkono sera za utawala haramu wa Israel zitagonga mwamba tu.
Kadhalika harakati hiyo ya Kiislamu ya Palestina imefafanua katika taarifa hiyo ya leo kuwa, wimbi la malalamiko mitandaoni baada ya Google na Apple kuiondoa Palestina katika ramani ya dunia ndani na nje ya Palestina linaonyesha wazi kuwa, kadhia ya Palestina ni ya kimataifa na jamii ya kimataifa ina imani nayo.
Siku ya Ijumaa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilieleza pia juu ya kughadhabishwa mno na kitendo hicho ghalati cha mashirika ya Google na Apple.
Maelfu ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ndani na nje ya Palestina wametumia hashtagi za #IacheHuruPalestina na #SimamaNaPalestina kuyakashifu na kuyashutumu vikali mashirika hayo ya Kimarekani kwa hatua yao hiyo ya kichokozi na kichochezi.
Google na Apple zilichukua hatua hiyo ya kifidhuli Jumanne iliyopita, ambapo mbali na kuondoa neno Palestina katika ramani zake zote za dunia, lakini pia yameyaarifisha maeneo mawili ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, kama sehemu za Israel.