Serikali ya Afghanistan: Taliban katu haitashinda vita wala haitaidhibiti nchi
Makamu wa Pili wa Rais wa Afghanistan amesisitiza kuwa, kundi la Taliban katu halitashinda katika vita vya nchi hiyo.
Sarwar Danesh ametoa sisitizo hilo katika ujumbe kwa mnasaba wa kuwadia Sikukuu ya Idul-Adhha na akabainisha kwamba, Taliban inadhani imeshinda katika vita vya Afghanistan na inaweza kuidhibiti na kuitawala nchi hiyo.
Hivi karibuni, kinara wa kundi la Taliban Mullah Haibatullah alisikika akisema kuwa, kundi hilo linakaribia kuasisi utawala wa Kiislamu nchini Afghanistan.
Akitoa jibu kuhusiana na kauli hiyo ya Mullla Haibatullah, Sarwar Danesh amesema, wananchi wa Afghanistan na Taliban inapasa waelewe kwamba ndoto hiyo liliyonayo kundi hilo kamwe haitathibiti na mfumo wa Jamhuri, tunu zilizobainishwa katika katiba ya Afghanistan na mafanikio yaliyopatikana nchini humo katika miongo miwili ya karibuni haviwezi kufanyiwa muamala wa aina yoyote.
Wakati huohuo Idara ya Usalama wa Taifa ya Afghanistan imeeleza katika taarifa kwamba, makundi ya kigaidi yenye makao yao nchini Pakistan yamekusudia kufanya hujuma za kigaidi ndani ya ardhi ya Afghanistan ili kuvuruga mchakato wa mazungumzo ya kutafuta suluhu na amani kati ya mirengo ya Waafghani na kundi la Taliban.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, makundi ya ukufurishaji yaliyoko Pakistan hayatishii uthabiti wa Afghanistan na eneo pekee, bali yanahatarisha pia amani na usalama wa dunia nzima.
Wiki iliyopita Umoj awa Mataifa ulieleza katika ripoti kuwa, kuna wanamgambo wapatao 600 wa mtandao wa kitakfiri wa Al Qaeda wanaoendesha harakati zao katika mikoa 12 ya Afghanistan na kwamba kinara wa mtandao huo Ayman Adh-Dhawahiri yuko katika moja ya mikoa hiyo.../