Hamas yauonya utawala wa Kizayuni kuhusu chokochoko Ghaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu chokochoko zake katika Ukanda wa Ghaza.
Ndege za utawala wa Kizayuni Jumapili usiku zililenga kituo cha wanampambano katika eneo la Bait Lahya, mashariki mwa Ukanda wa Ghaza.
Kufuatia uchokozi huo, Mahmoud Azahar, kiongozi wa ngazi za juu katika Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amewaonya vikali Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Utawal wa Kizayuni, Benny Gantz waziri wa vita wa utawala huo na Aviv Kochavi kamanda mkuu wa majeshi ya utawala huo kuwa, hujuma yoyote ya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza itakuwa na madhara mabaya kwa Israel.
Wakati huo huo, msemaji wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel amedai kuwa, ndege za kivita za utawala huo zimeshambulia kituo cha Hamas huko Ghaza katika kujibu hatua ya kutumwa baloni za moto kutoka Ghaza ambazo zimeelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yaani Israel.
Katika miezi ya hivi karibuni utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitekeleza mashambulizi dhidi ya Ghaza kwa kutumia mizinga, ndege za kivita, helikopta na droni ambapo hadi sasa melefu ya Wapalestina wameuawa shahidi au kujeruhiwa.
Tokea mwaka 2006, eneo la Ukanda wa Ghaza limekuwa chini ya mzingiro wa Israel wa nchi kavu, angani na baharini jambo ambalo limewasababishia wakaazi wa eneo hilo matatizo makubwa.