Malengo ya safari ya Mustafa al Kadhimi nchini Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i62918-malengo_ya_safari_ya_mustafa_al_kadhimi_nchini_marekani
Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi amewasili Washington kwa safari ya kikazi ya siku mbili na leo Alkhamisi tarehe 20 Agosti alitazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Donald Trump wa Marekani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 20, 2020 08:00 UTC
  • Malengo ya safari ya Mustafa al Kadhimi nchini Marekani

Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhimi amewasili Washington kwa safari ya kikazi ya siku mbili na leo Alkhamisi tarehe 20 Agosti alitazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Donald Trump wa Marekani.

Kunajitokeza swali kwamba, safari hii ya al Kadhimi nchini Marekani inafanyika kwa malengo gani?

Katika safari hii Waziri Mkuu wa Iraq atajadiliana na Rais wa Marekani kuhusu uhusiano wa pande mbili na masuala ya kanda ya magharibi mwa Asia. Kuhusu uhusiano wa pande mbili, kadhia ya kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ndiyo ajenda kuu ya mazungumzo hayo. Tarehe 5 Januari mwaka huu Bunge la Iraq lilipasisha muswada wa kuwafukuza wanajeshi wote wa Marekani katika ardhi ya Iraq. Tarehe 24 mwezi huo huo wa Januari mamilioni ya Wairaqi walifanya maandamano wakitaka kuondoka wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. Hata hivyo Marekani inafanya jitihada za kubakisha wanajeshi wake katika ardhi ya Iraq kwa kutumia vitisho vya vikwazo na kuzidisha matatizo ya kiuchumi ya Iraq ambayo ndio tatizo kubwa zaidi la sasa la nchi hiyo. 

Mwezi Juni mwaka huu Iraq na Marekani zilifanya mazungumzo yaliyojadili uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Iraq. Mazungumzo hayo hayakuwa na matunda ya kuridhisha. Hivyo inaonekana kuwa, katika safari ya sasa ya Waziri Mkuu wa Iraq mjini Washington suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Iraq litapewa tena kipaumbele katika mazungumzo ya pande hizo mbili. Wakati huo huo baadhi ya wabunge wa Iraq wametahadharisha kuwa, iwapo Waziri Mkuu Mustafa al Kadhimi ataafiki suala la kuendelea kuwepo wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo, Bunge litamtimua na kumuuzulu.

Suala jingine linalohusiana na pande hizo mbili ni matatizo ya kiuchumi ya Iraq. Nchi hiyo inasumbuliwa na matatizo mengi ya kiuchumi na hapana shaka kuwa miongoni mwa sababu za maandamano yaliyokuwa yakifanyika dhidi ya serikali iliyojiuzulu ya Adil Abdul Mahdi ni matatizo ya kiuchumi ya Iraq. 

Trump atamuomba al Kadhimi apunguze uhusiano na Iran

Mustafa al Kadhimi ana wasiwasi wa kuanza tena maandamano ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi kama yale yaliyofanyika wiki chache zilizopita dhidi ya serikali yake. Hivyo inatarajiwa kwamba, katika mazungumzo yake na viongozi wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump, Waziri Mkuu wa Iraq ataomba msaada wa kupunguza matatizo ya kiuchumi ya nchi yake.

Masuala ya kiusalama pia ni miongoni mwa mambo yatakayokuwa katika ajenda ya mazungumzo ya al Kadhimi na Donald Trump. Marekani ambayo inaendelea kushuhudia ongezeko la vitisho dhidi ya ubalozi na vituo vyake vya kijeshi nchini Iraq, itamuomba al Kadhimi kubana harakati za makundi ya mapambano nchini humo. Katika upande mwingine Waziri Mkuu huyo wa Iraq anaelewa vyema kwamba, makabiliano ya aina yoyote baina ya serikali na makundi ya mapambano yatakuwa na taathira mbaya katika hatima ya serikali yake na katika uchaguzi wa mapema wa Bunge uliopangwa kufanyika mwakani. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, itakuwa vigumu sana kwa pande hizo mbili kufikia mapatano katika kadhia hii.

Kuna masuala kadhaa ya kikanda pia ambayo yatamulikwa na kujadiliwa katika mazungumzo ya Waziri Mkuu wa Iraq na Rais wa Marekani mjini Washington. Miongoni mwa masuala hayo ni uhusiano wa Baghdad na Tehran. Serikali ya Marekani ambayo imefeli na kugonga mwamba katika sera zake za mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, inaishinikiza serikali ya Iraq ili ipunguze kiwango cha uhusiano wake na Iran.

Al Kadhimi akizunguzma na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Tehran

Safari ya sasa ya al Kadhimi nchini Marekani inafanyika kabla ya uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. Trump anafanya jitihada za kutumia safari hiyo na mazungumzo ya pande mbili kwa malengo ya kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, lakini inaonekana kuwa, Waziri Mkuu wa Iraq hatakuwa na jambo muhimu zaidi la kumpa au kumwahidi Donald Trump kuhusu suala la kupunguza uhusiano wa Baghdad na Tehran.

Iraq ina mpaka mkubwa zaidi wa kijiografia na Iran, na katika upande wa uchumi hasa katika kudhamini nishati ya umeme, ina haja kubwa sana ya kuimarisha uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu. Suala hili pia lilitiliwa mkazo na al Kadhimi mwenyewe wakati wa safari yake ya mwezi uliopita mjini Tehran.