Allawi atahadharisha kuhusu njama za Marekani dhidi ya Iraq
-
Iyad Allawi
Mkuu wa Muungano wa al Wataniya wa Iraq amesema kuwa Marekani ikishirikiana na Uingereza na Ufaransa, inaongoza njama dhidi ya Iraq kwa kisingizio cha muungano wa kimataifa dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.
Iyad Allawi amesema kuwa Uturuki pia inataka kuzusha machafuko nchini Iraq kwa kuwaunga mkono wanamgambo wenye silaha wa ndani ya Iraq na baadhi ya makundi ya kisiasa.
Mkuu wa Muungano wa al Wataniya wa Iraq ameongeza kuwa, katika miaka kadhaa ya hivi karibuni nchi hizo zimekuwa zikifanya mikakati ya kuisambaratisha Iraq kwa njia mbalimbali.
Habari nyingine zinasema kuwa, katika mlolongo wa maandamano yanayoendelea kufanywa na wananchi wa Iraq, wafanyakazi wa Wizara ya Umeme jana Jumapili waliivamia Wizara ya Fedha ya nchi hiyo mjini Baghdad na kufunga barabara kuu ya mji mkuu huo wakilalamikia kutolipwa mishahara yao.
Maandamano hayo ambayo yaliyoanza Oktoba Mosi mwaka jana kupinga ufisadi na ukosefu wa ajira katika mikoa ya kati na kusini mwa Iraq yangali yanaendelea.