HAMAS: Kuendelea ujenzi haramu wa vitongoji kumekashifu uongo wa Waarabu wafanyamapatano
Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuidhinisha mradi wa ujenzi wa maelfu ya nyumba mpya katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ni ithibati ya uongo wa madai uliyotoa utawala huo ya kusitisha mpango wake wa kulimega eneo hilo.
Hazem Qassim amesisitiza kuwa, kitendo kilichofanywa na tawala za Kiarabu cha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Kizayuni kimeuhamasisha zaidi utawala huo kuendeleza ujenzi haramu wa vitongoji katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Msemaji wa Hamas amebainisha kuwa, kupitishwa mradi wa ujenzi wa nyumba mpya katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kumekashifu na kuuanika hadharani uongo wa Waarabu wafanyamapatano.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel siku ya Alkhamisi vilitangaza kuwa, Waziri Mkuu wa utawala huo haramu Benjamin Netanyahu ameafiki mpango wa kujengwa nyumba mpya elfu tano katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye eneo la Ufukwe wa Magharibi.
Ripoti ya vyombo hivyo vya habari vya Kizayuni imeongeza kuwa, mnamo mwezi Februari mwaka huu Netanyahu alisitisha mpango huo wa ujenzi wa vitongoji kwa lengo la kuepusha hatua hiyo isije ikatibua makubaliano ya mapatano yaliyokuwa yamepangwa kusainiwa baina ya Israel na Imarati na Bahrain.
Hayo yanaripotiwa wakati Imarati ilisikika ikidai mara kadhaa kwamba, kusitishwa mpango wa kulimega eneo la Ufukwe wa Magharibi na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni sehemu ya makubaliano ya mapatano kati yake na utawala haramu wa Israel.../