Mahmoud Abbas autaka Umoja wa Mataifa uilinde Palestina
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, kadhia ya Palestina ni mtihani mkubwa kwa Umoja wa Mataifa wa kuthibitisha heshima na itibari yake.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Mahmoud Abbas akisema hayo jana na kuongeza kuwa, Umoja wa Mataifa unapaswa kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya kupatikana utatuzi wa amani wa kadhia ya Palestina kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameongeza kuwa, taifa la Palestina linauomba Umoja wa Mataifa ulilindie haki zake kutokana na utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani kukanyaga miongozo ya Umoja wa Mataifa na maazimio ya kimataifa na kuzidisha mashambulizi na jinai zao dhidi ya Wapalestina.
Amesema, taifa la Palestina limeweka matumaini yake kwa Umoja wa Mataifa na linataraji kukiona chombo hicho kikubwa zaidi cha kimataifa duniani kinaunga mkono mapambano ya haki ya wananchi wa Palestina ya kupigania uhuru na ukombozi wa haki zao.
Kabla ya hapo pia, Rais wa Mamlaka wa Ndani ya Palestina alikuwa amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuitisha mkutano wa kutafuta njia za kupatikana amani ya kweli. Mahmoud Abbas ameomba mkutano huo wa kimataifa ufanyike mwanzoni mwa mwaka ujao wa 2021.