Malengo ya Marekani ya kuwasilisha mpango wa kufunga ubalozi wake Baghdad
Serikali ya Marekani imetangaza mpango wa kufunga ubalozi wake katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad kutokana na kuendelea mashambulizi ya maroketi dhidi ya ubalozi huo.
Lakini pamoja na kuwepo tangazo hilo, haielekei kuwa Marekani itatekeleza kivitendo mpango huo. Iraq ina umuhimu mkubwa wa kijiopolitiki kwa Marekani. Kimsingi hujuma ya Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003 ilitekelezwa kwa sababu za kijiopolitiki.
Kwa mujibu wa takwimu za OPEC, Iraq ina akiba ya mapipa bilioni 145 ya petroli. Aidha Iraq huzalisha zaidi ya mapipa milioni 4.5 ya mafuta ya petroli kila siku na yanayouzwa nje ya nchi ni takribani mapipa milioni 4. Kuna ushahidi unaoonyesha kuwa, moja ya sababu za vita vya Marekani dhidi ya Iraq mwaka 2003 ni kwa ajili ya kupora utajiri wa mafuta ya nchi hii ya Asia Magharibi.
Baada ya kupita miaka 17 ya vita hivyo, mashirika kadhaa ya Marekani yamewekeza katika sekta ya mafuta nchini Iraq. Mwezi Agosti Ihsan Abdul Jabbar Ismael, Waziri wa Mafuta wa Iraq alitia saini mkataba na shirika la mafuta la Chevron la Marekani kuhusu uchumbaji na uzalishaji mafuta katika mkoa wa Dhi Qar. Waziri wa mafuta wa Iraq alisema: "Wizara ya mafuta inaendelea kufanya mazungumzo na shirika la Exxon Mobil kwa ajili ya miradi ya mafuta kusini mwa Iraq ambayo thamani yake ni makumi ya mabilioni ya dola."
Mbali na hayo, kutokana na kupakana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq ina umuhimu mkubwa sana kwa Marekani. Iraq ina mpaka wa pamoja na Iran wenye urefu wa zaidi ya kilomitta 1500. Moja kati ya malengo makuu ya uwepo wa Marekani Asia Magharibi au Mashariki ya Kati ni kuiweka chini ya darubini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na kudhoofisha hadhi na nafasi ya Tehran na waitifaki wake katika eneo.
Hivyo tangazo la kutaka kufungwa ubalozi wa Marekani mjini Baghdad linakinzana kikamilifu na malengo hayo ya Washington na ni kwa sababu hii ndio weledi wa mambo wakasema haielekei iwapo kweli Marekani itatekeleza kivitendo tishio lake la kufunga ubalozi wake mjini Baghdad au wala.
Inavyoelekea ni kuwa Marekani imetangaza mpango wa kufunga ubalozi wake mjini Baghdad ili kwa njia hiyo iweze kuishinikiza serikali ya Iraq kwa ajili ya kufikia malengo yake. Samir Abid, mchambuzi wa masuala ya kistratijia nchini Iraq anaamini kuwa, ubalozi wa Marekani ni sehemu ya Wizara ya Ulinzi, Pentagon. Anasema ubalozi huo umegharimu dola milioni 750 na thamani yake sasa inapindukia dola bilioni 10.
Afisa mmoja wa Marekani imesema nchi hiyo itapata hasara ikiamua kuondoka Iraq.
Hivi sasa Marekani ina matakwa matatu ambayo inataka serikali ya Iraq iyatekeleze. Kwanza ni kudhoofisha au kudhibiti makundi ambayo yako dhidi ya Marekani. Pili ni kudhamini usalama wa wanajeshi wa Marekani na tatu ni kukabiliana na ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo.
Aqil ar Radini, kiongozi wa muungano wa Nasr wa Iraq anafafanua kuhusu kadhia hii kwa kusema: "Marekani inamshinikiza waziri mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi ili aweze kudhibiti silaha zote ambazo haziko mikononi mwa serikali. Ni kwa msingi huo ndio katika siku za hivi karibuni Marekani ikatangaza kuwa inataka kufunga ubalozi wake Baghdad."
Marekani imekasirishwa na hujuma za mara kwa mara za maroketi dhidi ya ubalozi wake mjini Baghdad na kusema itaufunga ubalozi huo huku ikifungamanisha mashambulizi hayo na makundi ya muqawama yaliyo karibu na Iran. Hii ni katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni ofisi zote za kidiplomasia za Iran nchini Iraq zimekuwa zikishambuliwa. Balozi ndogo za Iran Najaf na pia Basra zimewahi kushambuliwa na kuteketezwa moto.
Ukweli ni kuwa, hujuma dhidi ya ubalozi na vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Iraq ni natija ya Washington kukiuka mamlaka ya kujitawala Iraq. Kilele cha ukiukwaji huo kilikuwa ni kuuawa kigaidi Shahidi Qasem Soleimani wakati akiwa kamanda mkuu wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq walipokuwa katika Uwanja wa Ndege wa Baghdad. Wawili hao na wale wote waliokuwa wameandamana nao waliuawa kinyama katika hujuma ya jeshi la kigaidi la Marekani na Rais Trump wa Marekani pia amekiri wazi kuhusika na hujuma hiyo iliyotekelezwa kinyume cha sheria.