Mitazamo miwili kuhusiana na matukio ya usalama nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63861-mitazamo_miwili_kuhusiana_na_matukio_ya_usalama_nchini_iraq
Katika majuma ya hivi karibuni Iraq imeshuhudia mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya ubalozi wa Marekani na vile vile mashambulio ya Washington dhidi ya ngome za Harakati ya Wananchi ya Hashd al-Shaabi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 06, 2020 12:51 UTC
  • Mitazamo miwili kuhusiana na matukio ya usalama nchini Iraq

Katika majuma ya hivi karibuni Iraq imeshuhudia mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya ubalozi wa Marekani na vile vile mashambulio ya Washington dhidi ya ngome za Harakati ya Wananchi ya Hashd al-Shaabi.

Kuna mitazamo miwili kuhusiana na mashambulio hayo ya wiki za karibuni. Mtazamo wa kwanza ni kuwa, baadhi ya makundi yaliyoanzishwa hivi karibuni na ambayo yanafanya harakati zao chini ya mjumuiko wa Hashd al-Shaabi yamekuwa yakifanya mashambulio dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.  Sababu ya hilo ni kuwa, Marekani ilimuua shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na Abu Mahdi al-Mohandes aliyekuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi la Hashd al-Shaabi.

Kwa upande mmoja Iran inaona kuwa kuondoka majeshi ya Marekani nchini Iraq ni kulipiza kisasi cha mauaji ya Qassim Suleimani, na katika upande mwingine makundi ya muqawama ya Iraq yanaona kuwa, hatua za Marekani nchini humo zinakiuka wazi mamlaka ya kujitawala nchi hiyo na ndio maana yanasisita kuondolewa majeshi ya Marekani nchini humo.

Wapiganaji wa Harakati ya Kujitolea ya wananchi ya Hashd Shaabi

 

Kwa kuzingatia hali hii, baadhi wanasema kuwa, mashambulio dhidi ya vituo vya kijeshi na ubalozi wa Marekani mjini Baghdad yanafanywa na makundi ya muqawama ili sambamba na kuongeza vitisho viilazimishe Marekani iondoe majeshi yake kutoka katika nchi hiyo.  Mtazamo huu una wafuasi ndani ya serikali ya Baghdad.

Ni kwa msingi huo ndio maana katika safari yake ya hivi karibuni hapa mjini Tehran Fuad Hussein, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq  akaitaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iyakinaishe makundi ya Iraq yaliyo karibu nayo yahitimishe mashambulio yake dhidi ya Marekani. Hata hivyo Tehran sambamba na kupinga mtazamo huo imetangaza kuwa, haiingilii masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Mtazamo wa pili ni kwamba, kimsingi kile kinachotokea hivi sasa nchini Iraq na mashambulio dhidi ya maeneo ya kidiplomasia ya mataifa mengine, yanafanywa na vibaraka na mamluki wa Marekani.

Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq

 

Wafuasi wa mtazamo huu wanasema kuwa, Marekani inatafuta kisingizio cha kuendelea kuweko kwake kinyume cha sheria nchini Iraq na hivyo kupuuza kabisa muswada wa Bunge la Iraq na takwa kuu la wananchi wa nchi hiyo la kuondoka nchini humo majeshi ya Marekani.

Wakati huo huo, waungaji mkono wa mtazamo huu wanasema kuwa, mamluki wa ndani wa Marekani ndio wanaotekeleza mashambulio hayo ili kwa upande mmoja watetereshe nafasi ya makundi ya muqawama mbele ya macho ya wananchi wa Iraq na kuyaonyesha kuwa ndio chanzo cha ukosefu wa amani na usalama; na kwa upande wa pili walete mpasuko baina ya serikali na makundi ya muqawama na kisha kukuza mpasuko huo. Katika uwanja huo, tayari kunazungumziwa madai ya uwezekano wa makundi ya muqawama kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi.

Kuhusiana na hilo, Kazem al-Fartousi, msemaji wa Brigedi ya Sayyid Shohada inayofungamana na Hashd al-Shaabi anasema: Kuna nyaraka zinazothibitisha kwamba, ubalozi wa Marekani kupitia mamluki wake umekuwa ukifanya mashambulio ya maroketi dhidi ya maeneo ya kidiplomasia ukiwemo ubalozi wake mjini Baghdad. Hii ni kutokana na kuwa, Marekani inataka kuvuruga hali ya usalama ya Iraq na kuziathiri fikra za waliowengi nchini humo.

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa iIaq

 

Abu Ali al-Basri, Naibu Mkuu wa Operesheni za Hashd al-Shaabi sambamba na kuashiria kwamba, mashambulio ya makombora dhidi ya baadhi ya maeneo mjini Baghdad ni kisingizo cha Marekani cha kutaka kubakia kijeshi katika nchi hiyo amesisitiza kuwa, harakati ya wananchi ya Hashd al-Shaabi haihusiki kwa namna yoyote ile na maashambulio dhidi ya balozi na maeneo ya kidiplomasia na katu haijapanga mipango ya jambo hilo.

Nukta ya mwisho ni kuwa, licha ya kuwa makundi ya muqawama hayaridhishwi na uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq na yanaitambua hatua hiyo kwamba, inakiuka mamlaka ya kujitawala Baghdad na yamefanya mashambulio dhidi ya ngome na vituo vya kijeshi vya Marekani, lakini makundi hayo yanapinga na kukanusha vikali madai ya kuhusika kwao na mashambulio dhidi ya maeneo ya kidiplomasia. Inaonekana kuwa, kile ambacho kinajiri hivi sasa nchini Iraq kinalenga kuhairibu haiba ya makundi ya muqawama na hilo kuwa na taathira kwa uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanyika mwezi Juni mwaka ujao wa 2021.