Mwalimu Mpalestina mkazi wa Ghaza achaguliwa mwalimu bora duniani
Bi Asma Mustafa, mwalimu wa kike wa shule ya wasichana ya "Halima al Saadiyah" ya kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza huko Paletina ameshinda tunzo ya mwalimu boda duniani mwaka huu wa 2020 ijulikanayo kwa jina la AKS Education Award.
Bi Asma Mustafa ni mwalimu wa lugha ya Kiingereza wa skuli hiyo ya wasichama na amepata tunzo hiyo ya mwalimu bora duniani baada ya kuwashinda washiriki wengi wa mashindano ya tunzo hiyo. Amepata ushindi huo wa kupigiwa mfano kutokana na ubunifu wake katika usomeshaji na utunzi wa vitabu ikiwemo michezo 45 ya ufundishaji wa lugha ya Kiingereza kwa watu ambao Kiingereza si lugha yao ya asili.
Mwalimu huyo Mpalestina ni mwanachama wa taasisi nyingi za kimataifa za elimu na anafanya kazi pia na mashirika mbalimbali ya kimataifa kama vile Microsoft, Google, Apple na National Geographic.

Jumuiya ya AKS Education ya nchini India mwaka jana pia ilitangaza majina ya walimu 100 bora duniani kutoka nchi 72 tofauti. Miongoni mwa walimu hao bora ni Ayad Ahmad al Sufi mwalimu Mpalestina wa mjini Jenin, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kutokana na kazi kubwa ya kuyaingiza masomo katika mfumo wa kidijitali.
Rana Ziyada, mwalimu mwingine Mpalestina mkazi wa Ukanda wa Ghaza naye alikuwa miongoni mwa walimu 50 bora duniani mwaka 2018.
Licha ya kuzingirwa kila upande na kufanyiwa ukandamizaji mkubwa mno na utawala dhalimu wa Israel, lakini Wapalestina daima wamekuwa wakitia fora katika masuala ya elimu.