Umoja wa Mataifa wataka kusitishwa mivutano huko al Hudaydah, Yemen
Mkuu wa Timu ya Uangalizi ya Umoja wa Mataifa huko Yemen ametaka kutekelezwa usitishaji vita katika mji wa al Hudaydah magharibi mwa nchi hiyo sambamba na kusitishwa mivutano katika eneo hilo.
Abhijit Guha jana Jumatatu alieleza kutiwa wasiwasi na mashambulizi ya karibuni huko Yemen na kueleza kuwa wakati umefika sasa wa kusitishwa mapigao na mivutano ya kijeshi nchini humo.
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, mji wa al Hudaydah wiki iliyopita ulikumbwa na mashambulizi ya anga na nchi kavu ambapo mada za milipuko zilitumika katika mashambulio hayo. Amesema kuuliwa raia wakiwemo watoto wadogo wa Kiyemeni katika mashambulizi hayo ni jambo linalotia wasiwasi.
Guha amesisitiza kuwa, Timu ya Uangalizi ya Umoja wa Mataifa itaendelea kuzungumza na pande zinazozozana ili kufanikisha usitishaji vita.
Aidha katika mazungumzo yake ya karibuni na Abhijit Guha, Muhammad Isays Fahim Gavana wa al Hudaydah amesema kuwa muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia umekiuka mapatano hayo zaidi ya mara elfu 30 licha ya Sana'a kuheshimu mapatano hayo ya kusimamisha mapigano yaliyofikiwa huko Sweden.