Kuzingirwa Gaza na taathira zake katika kuenea corona
Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza ambao unaendelea kuzingirwa pande zote na utawala ghasibu wa Israel, imetangaza kwamba maabara makuu ya ukanda huo yamefungwa kutokana na kutokuwa na suhula na vifaa vya kufanyia vipimo vya corona.
Corona ni maradhi ya kuambukiza yanayoenea kwa kasi kubwa ambapo kufikia sasa yamepelekea watu karibu milioni 67.5 duniani kuambukizwa na wengine zaidi ya milioni 1.55 kupoteza maisha. Palestina kama zilivyo nchi nyingine za dunia imeathirika na ugonjwa huo hatari na kufikia sasa watu wapatao 110,000 wameambukizwa na wengine 900 kupoteza maisha. Kati ya idadi hiyo, watu 25,121 wanaoishi katika Ukanda wa Gaza wameathirika na wengine 140 wamekufa ambapo hali ya 170 wako katika hali mahututi.
Pamoja na hali hiyo, tofauti kubwa iliyopo kati ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni kuwa tokea mwaka 2006 Ukanda wa Gaza unakabiliwa na mzingiro mkali wa utawala ghasibu wa Israel na hivyo kutokuwepo uwezekano wa kupelekwa huko misaada ya kibinadamu yakiwemo madawa na vifaa vya afya na matibabu. Ni kutokana na ukweli huo mchungu ndipo Wizara ya Afya ya Gaza ikatangaza kuwa kuzuiwa mashine na vifaa vya kitiba kuingizwa katika ukanda huo, kumehatarisha mfumo wake mzima wa afya. Ni kwa sababu hiyo pia ndipo maabara makuu ya ukanda huo yakafungwa.
Kuzingirwa Ukanda wa Gaza kwa miaka 14 kumekuwa na matokea mabaya mno kwa wakazi wake, ikiwa ni pamoja na kubadilika taratibu kuwa jela ya wazi, umasikini unaenea, wagonjwa wenye maradhi sugu wanaongezeka na kwa mujibu wa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ukanda huo unakaribia kushuhudia maafa makubwa ya kibinadamu. Pamoja na hayo ugonjwa wa corona ni ugonjwa tofauti kabisa. Hii ni kutokana na kuwa unaenea kwa kasi kubwa na kuua wahanga wake haraka sana.
Uhaba au kutokuwepo kabisa vifaa vya kitiba vya kugundua virusi au kuwapa matibabu wagonjwa wa corona kunaweza kuzuia juhudi za kupambana na ugonjwa huo na hivyo kuzidisha maafa ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza. Fat'hi Abu Warda, Mshauri wa Waziri wa Afya wa Palestina amesema kuwa hali ya afya katika Ukanda wa Gaza ni ya kutia wasi wasi mkubwa na kutahadharisha kwamba idadi ya walioambukizwa corona na kupoteza maisha katika mahospitali ya ukanda huo inazidi kuongezeka na kuwa dunia inapasa kusubiri kushuhudia maafa makubwa yakitokea katika ukanda huo wakati wowote.
Nukta nyingine ni kwamba licha ya kuwepo hali mbaya kama hiyo katika Ukanda wa Gaza lakini serikali ya Palestina bado inaendelea kujishughulisha na mivutano ya kisiasa na makundi ya ukanda huo na kukataa kabisa kutekeleza majukumu yake kuhusu watu wa ukanda huo ambao wanaendelea kushuhudia machungu ya mzingiro wa miaka mingi kutoka kwa utawala wa kibaguzi wa Israel.
Nchi tajiri za Kiarabu na hasa zile ambazo zimeamua kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo na vile vile madola makubwa yameamua kukaa kimya na kutochukua hatua yoyote ya kupunguza machungu hayo ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Hii ni katika hali ambayo Ashraf Qudrat, Msemaji wa Wizara ya Afya ya Palestina Katika Ukanda wa Gaza amezitaka pande za ndani, kieneo na kimataifa kutuma haraka iwezekanavyo misaada ya kibinadamu na kiafya katika ukanda huo.
Hali ya hivi sasa ya Ukanda wa Gaza na hasa katika mazingira haya ya kuenea virusi vya corona inathibitisha wazi kuwa madai ya kuheshimu haki za binadamu na kushughulikia matatizo mengine ya jamii ya mwanadamu ni nara na maneno matupu tu na kwamba maadili yamefutwa kabisa katika siasa za ulimwengu.