Dec 16, 2020 07:40 UTC
  • Mamlaka ya Ndani ya Palestina: Quds ni mstari wetu mwekundu

Mamlaka ya Ndani ya Palestina imesema kuwa Quds na matukufu yake ni mstari mwekundu wa Wapalestina.

Nabil Abu Rudeina Msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina jana usiku alisema kuwa hujuma na mashambulizi yanayofanywa na Wazayuni huko Quds inayokaliwa kwa mabavu, kupanuliwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi, kuutenganisha mji wa zamani wa Quds na vitongoji vyake na ardhi nyingine za Palestina zinatekelezwa kwa lengo la kukwamisha kuundwa nchi huru ya Palestina. 

Mji wa Quds huko Palestina unaokabiliwa na mashambulizi na hujuma za maghasibu wa Kizayuni 

Abu Rudeina amebainisha kuwa utawala wa Kizayuni umeendeleza hatua zake za upande mmoja za kichokozi na kuzishambulia karibu kaya 30 za Wapalestina wakazi wa Quds Mashariki khususan Sarwan na Sheikh al Jarrah; na una mpango wa kuwafukuza raia hao katika makazi yao; hatua itakayosababisha makumi ya raia wa Kipalestina kuwa wakimbizi. 

Afisa huyo wa Palestina ameeleza kuwa, Israel inashadidisha vitendo vyake haramu na kubadili muundo wa kijiografia na kijamii wa mji wa Quds sambamba na kufuta utambulisho na utamaduni wa Kiarabu kupitia mipango yake ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na miundomsingi inayohusiana na vitongoji hivyo ikiwemo na kujenga barabara na njia ya chini kwa chini.

Msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameitolea wito jamii ya kimataifa kuingilia kati na kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuuwajibisha na kuufikisha mbele ya vyombo vya sheria utawala ghasibu wa Israel kwa hujuma zake hizo.  

 

Tags