Oct 02, 2024 03:11 UTC
  • Jumatano, tarehe Pili Oktoba, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 28 Mfunguo Sita Rabiu Awwal 1446 Hijria mwafaka na tarehe Pili Oktoba 2024.

Siku kama ya leo miaka 837 iliyopita, kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria, mji wa Baitul-Muqaddas ulikombolewa na Salahuddin Ayyubi kamanda mwanamapambano wa Kiislamu.

Awamu ya kwanza ya Vita vya Msalaba baina ya Wakristo na Waislamu vilianza 1096 ambapo miaka minne baadaye majeshi ya Msalaba yalishambulia mji wa Baitul-Muqaddas na kuukalia kwa mabavu. Wanajeshi hao wa Msalaba walifanya uporaji na kuwauwa kikatili maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia wa ardhi hiyo. Hata hivyo mnamo mwaka 1187, baada ya Salahuddin Ayyubi kudhibiti Syria, Lebanon na Misri, aliuzingira mji wa Baitul-Muqaddas.

Awali aliwatumia ujumbe wavamizi akiwaeleza heshima maalumu aliyonayo kwa mji huo na kutotaka kufanya umwagaji damu katika eneo hilo na kuwataka wavamizi hao waondoke katika mji huo na hata akawadhaminia usalama wa mali zao. Hata hivyo wapiganaji wa msalaba walikataa na hivyo kupelekea kuibuka vita na mji huo kukombolewa na Waislamu katika siku kama ya leo wakiongozwa na kamanda Salahuddin Ayyubi. 

Miaka 155 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Mahatma Gandhi, kiongozi wa harakati ya kupigania uhuru nchini India katika moja ya vijiji vya jimbo la Gujarat.

Mwaka 1891 Gandhi alirejea kutoka nchini Uingereza na kuishi mjini Mumbai. Mwaka 1893 Mahatma Gandhi alielekea mjini KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini. Akiwa huko alishuhudia ubaguzi wa rangi wa jamii ya wachache ndani ya taifa hilo. Mwaka 1917 na baada ya kurejea nchini kwake alipata umashuhuri mkubwa.

Miaka michache baada ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia yaani akiwa na umri wa miaka 33 aliongoza mapambano kwa ajili ya kuwaokoa watu wake sanjari na kupigania uhuru wa India kutoka mikononi mwa Waingereza, na hatimaye alifanikiwa kulipatia uhuru taifa hilo hapo mwaka 1947 baada ya kustahamili matatizo mengi akiwa na wanamapambano wengine kama Jawaharlal Nehru .

Mahatma Gandhi

Tarehe Pili Oktoba miaka 120 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake, na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene ameacha vitabu vingi kkama 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na 'Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

Graham Greene

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na mwanzoni mwa karne ya 19, Wafaransa walipata satua zaidi nchini humo. Mwaka 1849 nchi hiyo ilikoloniwa rasmi na Ufaransa.

Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

Na siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, baada ya Imam Khomeini MA kuzuiwa kuendesha shughuli za kisiasa na kidini huko Iraq na kwa kuzingatia kuwa utawala wa zamani wa wakati huo wa Iraq ulikuwa ukikabiliana na mapambano ya Imam Khomeini na kuweka vizuizi vikubwa, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliamua kuondoka Iraq na kuelekea Kuwait.

Hata hivyo serikali ya Kuwait ilimzuia Imam kuingia nchini humo ili kulinda uhusiano wake na utawala wa Shah.

Kufuatia hatua hiyo, siku kadhaa baadaye Imam Khomeini MA akaelekea uhamishoni nchini Ufaransa.

Itakumbukwa kuwa, mienendo na vitendo visivyo vya kibinadamu vya utawala wa Baath wa Iraq vilizusha hasira za wananchi wa Iran ambao walikuwa katika siku muhimu za kupambana na utawala dhalimu wa Shah hapa nchini. 

Imam Khomeini akiwa Paris

 

Tags