Jan 16, 2025 02:35 UTC
  • Alkhamisi, Januari 16, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Rajab 1446 Hijria sawa na tarehe 16 Januari 2025.

Tarehe 15 Rajab miaka 1451 iliyopita kundi la kwanza la Waislamu lilianza safari ya kuondoka Makka na kuhamia Uhabeshi, barani Afrika.

Hijra hiyo iliyokuwa na taathira kubwa katika harakati za Uislamu ilifanyika miaka 8 kabla ya Mtume (saw) kuhamia Madina.

Baada ya kushadidi mashaka ya Waislamu waliokuwa wakiteswa na kusumbuliwa na washirikina wa Makka, Mtume Muhammad (saw) aliwaamuru baadhi ya maswahaba zake waelekee katika ardhi ya Uhabeshi barani Afrika kwa ajili ya kujilinda na adha na mateso ya washirikina.

Kundi hilo la Waislamu lililojumuisha wanaume 11 na wanawake 4 likiongozwa na Uthman bin Madh'un, lilihamia Uhabeshi na kutayarisha uwanja na mazingira mazuri ya Hijra ya pili ya Waislamu kuelekea katika ardhi hiyo ya Afrika. Kundi hilo la pili liliongozwa na binamu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ja'far bin Abi Twalib.

Hijra hizo mbili zilikuwa na mchango mkubwa wa kueneza zaidi dini ya Uislamu barani Afrika. 

Miaka 1444 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, Kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas. Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas. 

Masjidul ya Dhul Qiblatein, Madina

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Bibi Zaynab (AS) mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi. Bibi Zaynab AS alizaliwa mwaka wa 6 Hijiria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake Imam Ali AS na mama yake Bibi Fatimat Zahra AS. Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab AS alishiriki katika tukio la Karbala pamoja na kaka yake Imam Hussein AS na watu wengine wa familia ya Mtume SAW. Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake.   

Haram ya Bibi Zainab, Damascus

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita mwafaka na tarehe 15 Rajab mwaka 60 Hijria, alifariki dunia Muawiyah bin Abu Sufiyan, adui mkubwa wa Ahlibaiti wa Mtume Muhammad (saw) na mwasisi wa utawala wa Bani Umayyah.

Muawiyah alizaliwa miaka 15 kabla ya kuhama Mtume SAW kutoka Makka na kuelekea Madina, na alisilimu wakati wa kukombolewa Makka na jeshi la Kiislamu katika mwaka wa 8 Hijria.

Muawiyah alishika Uliwali wa Sham wakati wa Ukhalifa wa Omar bin Khattab na wakati wa uongozi wa Imam Ali bin Abi Twalib (A.S) alianzisha vita vya Siffin kwa kisingizio cha kulipiza kisasi cha kuuawa Othman bin A'ffan.

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita yaani tarehe 16 Januari 2001, Rais Laurent Desire Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alipigwa risasi na mmoja wa walinzi wake katika ikulu ya Rais na kujeruhiwa vibaya.

Baada ya tukio hilo kulienea habari za kutatanisha juu ya hatima ya kiongozi huyo. Tarehe 18 Januari yaani siku mbili baadaye, serikali ya Kinshasa ilithibitisha kufariki dunia Rais Laurent Desire Kabila. Kabila alizaliwa mwaka 1939 huko Katanga na kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.

Aliingia madarakani mwaka 1997 baada ya vikosi vya askari aliokuwa akiwaongoza kuuteka mji wa Kinshasa na kumlazimisha Mobutu Sese Seko, rais wa wakati huo wa Zaire ya zamani kukimbilia nje ya nchi.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 179 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Januari 1846, vilianza vita baina ya Marekani na Mexico baada ya Washington kuishambulia nchi hiyo.

Vita hivyo vilivyochukua muda wa miaka miwili, vilitokea baada ya Marekani kudai kwamba wahajiri wa nchi hiyo wanateswa nchini Mexico. Hata hivyo ukweli ni kuwa, Marekani ilianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuyatwaa baadhi ya maeneo ya Mexico hususan eneo la Texas.

Katika vita hivyo, Marekani iliyakalia kwa mabavu majimbo ya Texas, California, Nevada, Utah, Arizona na New Mexico.   

Bendera ya Mexico

Tarehe 27 Dei miaka 69 iliyopita Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi akiwa pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini.

Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah.

Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.   

Sayyid Navvab Safavi