Utawala wa kiimla wa Saudia waendelea kukiuka haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i65232
Vikosi vya usalama vya Saudia vinaendeleza kampeni ya wazi wazi ya kukiuka haki za binadamu katika ufalme huo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 17, 2020 02:45 UTC
  • Utawala wa kiimla wa Saudia waendelea kukiuka haki za binadamu

Vikosi vya usalama vya Saudia vinaendeleza kampeni ya wazi wazi ya kukiuka haki za binadamu katika ufalme huo.

Watawala wa Saudi Arabia hawawezi kuvumilia hata kidogo haki za binadamu. Moja ya sababu ambazo zimepelekea watawala wa Saudia wasiruhusu uzingatiwaji haki za binadamu ni utambulisho wa mfumo wa utawala  nchini humo. Saudi Arabia inatawaliwa na ukoo wa Aal Saudi ambao  himaya yake ya kifikra ni idiolojia ya Uwahhabi. Mtindo wa utawala na wa maisha wa ukoo wa Aal Saud unaenda kinyume kabisa na matakwa ya raia wa nchi hiyo.

Ukoo wa Aal Saud unaamini kuwa wananchi hawana nafasi yoyote katika uendeshaji nchi na hivyo hakuna uchaguzi wa maana unaofanyika Saudia. Wananchi hawana nafasi hata kidogo katika kuainisha mfalme wa nchi hiyo. Wakati  wanawafalme wa Saudia wanaishi maisha ya raha mstarehe na anasa huku wakiwa na utajiri wa kupindukia, idadi kubwa ya Wasaudia wanaishi katika umasikini mkubwa, ukosefu wa ajira na ubaguzi rasmi. Mfumo wa utawala Saudia umepelekea kuibuka ufa mkubwa katika jamii na jambo hilo limekuwa cheche ya kujitokeza harakati kubwa ya malalamiko ya wananchi dhidi ya watawala.

Maandamano ya kumlaani bin Salman baada ya kuuawa kikatili Jamal Khashoggi

Pamoja na hayo Watawala wa Saudia hawawezi kustahamili hata kidogo ukosoaji na harakati za kiraia. Kwa msingi huo harakati yoyote au mtu yeyote anayekosoa au kupinga ufalme  anakabiliwa na ukandamizaji mkubwa na ukatili wa maafisa wa usalama nchini humo na wengi hata wamenyongwa. 

Hali imezidi kuwa mbaya nchini humo wakati Mohammad Bin Salman alipoteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme mnamo Januari 2015.

Mohammad Bin Salman hadi sasa ameamuru kukamatwa wapinzani  wakiwemo wasomi wengi wa Kiislamu, wanafikra, wahadhiri wa vyuo vikuu, watetezi wa haki za binadamu, wafanyabiashara mashuhuri na hata wanawafalme wa ukoo wa Aal Saud ambao wanapinga sera zake. Wanaoshikiliwa wanakabiliwa na tuhuma bandia za ufisadi.

Mbali na hayo, utawala dhalimu wa Saudia umezidisha ukandamizaji dhidi ya wananchi katika baadhi ya maeneo hasa eneo la mashariki mwa nchi hiyo. Sababu kuu ya kushadidi ukandamizaji mashariki mwa Saudia ni kuwa, asilimia 10 hadi 15 ya wenyeji wa eneo hilo ni Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao aghalabu wanaishi katika mkoa wa Ash Sharqiyah. Wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na ubaguzi unaotekelezwa kwa makusudi na watawala wa Saudia. Katika hatua ya hivi karibuni, vikosi vya kijeshi Saudia viliharibu nyumba za raia katika mji wa Qatif na kisha maafisa wa usalama wakawakamata vijana 34 na wahubiri wa Kiislamu mjini humo.

Janga la COVID-19 au corona Saudia pia limeandaa mazingira ya kukandamizwa zaidi wananchi na kukiukwa haki za binadamu. 

Kuhusiana na nukta hiyo, watetezi wa haki za binadamu wanasema kuwa mwezi Aprili utawala wa Saudia ulianzisha kamatakamata mpya wakati wananchi wakiwa wanajishughulisha na janga la corona. Imedokezwa kuwa katika kipindi hicho idadi kubwa ya waandishi habari, wahubiri wa Kiislamu na wahadhiri wa vyuo vikuu wanaoukosoa ufalme walikamatwa.

Nukta ya mwisho ambayo tunaweza kuashiri hapa ni kuwa, ukandamizaji huo unaotekelezwa na watawala dhalimu wa Saudia umeandamana na kimya kisicho cha kawaida cha taasisi za kimataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na madola ya Magharibi ambayo yanadai kutetea haki za binaadamu. Pamoja na hayo baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani yamekosoa ukiukwaji wa haki za binadamu Saudia na kunyongwa wafungwa wasio na hatia katika ufalme huo.

Lakini ukosoaji huo wa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu haujaweza kuilazimisha serikali ya Saudia ibadili sera zake katili hasa kutokana na kuwa wakuu wa Riyadh wanapata uungaji mkono wa madola makubwa ya kibeberu duniani. Kesi ya hivi karibuni kabisa ya ukosoaji ambayo Saudia imeipuuza ni ile ya Bi. Loujain Alhathloul.

Huyo ni mwanamke ambaye kosa lake ni kuwatetea wanawake wa Saudia ambao wanashikiliwa katika jela za kuogofya za ufalme huo huku wakikabiliwa na mateso makali na udhalilishaji wa kijinsia.  Pamoja na kuwa mashirika makubwa ya kutetea haki za binadamu duniani yameikosoa Saudia kwa kumkandamiza Loujain Alhathloul, lakini utawala wa Riyadh umepuuza ukosoaji huo na unaendelea kumshikilia.