Yemen: Hakuna mpango wowote wa amani uliopendekezwa kwa wakati huu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i67450-yemen_hakuna_mpango_wowote_wa_amani_uliopendekezwa_kwa_wakati_huu
Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amesema, hadi wakati huu hakuna mpango wowote wa suluhu na amani uliopendekezwa na nchi zingine na hakuna mpango wowote miongoni mwa iliyopendekezwa na serikali ya Sana'a uliokubaliwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 03, 2021 00:52 UTC
  • Yemen: Hakuna mpango wowote wa amani uliopendekezwa kwa wakati huu

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amesema, hadi wakati huu hakuna mpango wowote wa suluhu na amani uliopendekezwa na nchi zingine na hakuna mpango wowote miongoni mwa iliyopendekezwa na serikali ya Sana'a uliokubaliwa.

Muhammad Ali Al Houthi ameeleza kuwa, maadui wanajaribu kuonyesha kwamba operesheni ya Ma'rib iko nje ya vita vya Yemen na kwamba jeshi na kamati za wananchi ndio walioanza kuishambulia Ma'rib, ilhali kinachofanywa na vikosi vya Yemen ni kujitahidi kuikomboa Ma'rib kutoka kwenye makucha ya ukaliaji wa mabavu wa muungano vamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia.

Al Houthi amesisitiza pia kwamba, Sana'a inakaribisha wazo la kushiriki mazungumzo ya kutafuta suluhu na kufikia amani na nchi vamizi yaliyopendekezwa kufanyika nchini Russia.

Martin Griffiths

Kabla ya hapo, mkuu huyo wa kamati kuu ya mapinduzi ya Yemen aliukosoa Umoja wa Mataifa kwa kutokuwa na ratiba yoyote maalum na akasema, mjumbe wa UN Martin Griffiths hajapendekeza mpango wowote wa kutafuta suluhu ya vita vya Yemen.

Katika muda wa chini ya mwezi mmoja ujao, uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa na Saudia na washirika wake dhidi ya nchi masikini ya Kiarabu ya Yemen utaingia katika mwaka wake wa saba; na kwa muda wa miaka yote hii, nchi hiyo imewekewa mzingiro wa pande zote za nchi kavu, angani na baharini huku maelfu ya Wayemen wakiwa wameshauwa na kujeruhiwa hadi sasa na mamilioni ya wengine wakibaki kuwa wakimbizi.../